MBUNGE SHINGO AAPA KUIINUA UKONGA, AANZA MAFUNZO BURE KWA VIJANA 140
MBUNGE SHINGO AAPA KUIINUA UKONGA, AANZA MAFUNZO BURE KWA VIJANA 140
Mbunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Mhe Bakari Shingo, amesema amejipanga kuyatumikia kwa nguvu makundi yote ndani ya jimbo hilo, ikiwemo kuwainua vijana.
Shingo ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, pembezoni mwa hafla ya uapisho wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam iliyofanyika leo jijini humo.
Amesema yeye ni muumini wa kazi, na anaamini Jimbo la Ukonga litakuwa miongoni mwa majimbo yenye maendeleo makubwa nchini, na hatimaye kuwa mfano na maarufu kwa kufanya vizuri.
Ameeleza kuwa hapo jana alizindua utaratibu maalumu wa kuwawezesha vijana wa jimbo hilo, ambapo zaidi ya vijana 140 wa awamu ya kwanza watapatiwa mafunzo ya uendeshaji bodaboda na bajaji bila malipo. Mafunzo hayo yatawasaidia vijana kuendesha vyombo hivyo kwa kutambulika rasmi na mamlaka husika.
Mbunge Shingo amesema gharama za mafunzo hayo zitabebwa na yeye binafsi pamoja na marafiki zake ambao ni wadau mbalimbali.
Akizungumza kwa hisia, Shingo alisema:
“Ukiondoa roho mbaya, ubunge ni fursa. Ukilitumia vizuri, watu watanufaika nawe. Mimi sijaomba utajiri, nimeomba umaarufu, na umaarufu mzuri ni ule wa matendo mema. Hata nikifa, watu watanieleza kwa mema niliyowafanyia.”
Amesisitiza kuwa agenda za wananchi wa Ukonga lazima zitekelezwe ili kuleta maendeleo na kuhakikisha anawatumikia kikamilifu kama alivyowaahidi.
Aidha, Shingo amesema atazindua dawati maalumu la kusikiliza kero za wananchi kila wiki, ili kuhakikisha maoni, changamoto na mapendekezo ya wakazi wa Ukonga yanapokelewa moja kwa moja na kufanyiwa kazi kwa wakati. Amesema utaratibu huo utasaidia kuongeza uwazi na ushirikishwaji katika utendaji wake.
Pia ameahidi kuanza ziara maalumu katika mitaa yote ya Jimbo la Ukonga kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwashirikisha wananchi katika kupanga vipaumbele vya bajeti ya mwaka ujao. Kwa kufanya hivyo, amesema, atahakikisha wananchi wanahusishwa si tu kama watazamaji bali kama sehemu ya maamuzi.




Comments