NIDA YAZINDUA NAMBA MAALUM ITAKAYOWAWEZESHA WAOMBAJI KUFUATILIA TAARIFA ZA MAOMBI YAO
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imezindua namba maalum ya kutuma ujumbe mfupi wa simu bila malipo, 15274, itakayowawezesha wananchi kufuatilia kwa urahisi taarifa za maombi ya utambulisho wa Taifa popote walipo nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa namba hiyo Katika makao makuu ya NIDA Jijini Dar es Salaam amesema Serikali inaridhishwa na utendaji kazi wa NIDA katika kuimarisha utoaji wa huduma zake kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayomuwezesha mwananchi kupata taarifa zake za utambulisho wa taifa bila malipo.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza usumbufu unaotokana na ufuatiliaji wa huduma hizo katika ofisi za W za NIDA ngazi ya Wilaya huku akibainisha kwamba si mara ya kwanza kwa NIDA kuanzisha mifumo ya kisasa ya kidijitali ya kutoa huduma bora kwa watanzania.
Aidha Simbachawene Amesisitiza kuwa huduma hiyo itarahisisha upatikanaji wa taarifa, kupunguza gharama za usafiri kwa wananchi, kuondoa msongamano na foleni katika ofisi za NIDA ngazi ya wilaya pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za utambulisho wa taifa.
Hivi leo tunavyozungumza katika Wilaya zetu,viko vitambulisho vingi sana ambavyo havijachukuliwa na sababu kubwa inakua kwamba muombaji hajui kitambulisho chake kipo katika hatua gani,kupitia mfumo huu ambao ninauzindua utajibiwa na utaambiwa kama namba yako umepata ndani ya siku tano na kama ujapata ndani ya siku tano tangu ulipoomba ukitumia mfumo huu (15274) utajibiwa kwanini ujapata .” Amesema Waziri Simbachawene
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, ameeleza kwamba kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya wananchi kushindwa kwenda kuchukua vitambulisho vyao Katika ofisi za NIDA ngazi za wilaya hali inayosababisha kuwepo kwa mlundikano wa vitambulisho katika ofisi hizo.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa namba 15274 utamwezesha mwananchi kufahamu kwa urahisi hali ya maombi yake au kupata namba ya utambulisho wa Taifa endapo ameisahau, kwa kutuma ujumbe mfupi na kupokea majibu papo hapo, hatua itakayochangia kupunguza mrundikano wa vitambulisho na kuboresha huduma kwa wananchi.





Comments