UTT AMIS Yaongeza Wigo wa Uwekezaji, Mifuko yake yazidi kukua ,yawaita vijana kuwekeza
UTT AMIS Yaongeza Wigo wa Uwekezaji, Mifuko yake yazidi kukua
![]() |
| Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Serikali ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT AMIS), Simon Migangala, akizungumza katika mkutano wa mwaka wa taasisi hiyo. |
![]() |
| Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT AMIS, Profesa Faustin Kamuzora, akizungumza |
![]() |
| Baadhi ya wawekezaji kupitia UTT AMIS wakifuatilia taarifa mbalimbali za mwaka juu ya uwekezaji wao. |
Dar es Salaam, Desemba 19, 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Serikali ya Uwekezaji wa Pamoja (UTT AMIS), Simon Migangala, amesema taasisi hiyo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwawezesha Watanzania wa makundi yote kushiriki kikamilifu katika fursa za uwekezaji kupitia mifuko ya pamoja.
Migangala ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Mkutano wa Mwaka wa UTT AMIS, akibainisha kuwa licha ya kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji, bado Watanzania wengi hawajafikiwa na fursa za uwekezaji wa pamoja.
Amesema mkutano huo ni wa kwanza kwa wanachama wa Mfuko wa Umoja, ambao ulianzishwa mwaka 2005, ambapo umeonesha ukuaji mkubwa wa kifedha.
“Mfuko wa Umoja umeendelea kukua kwa kiwango kizuri sana. Ulianza na Shilingi bilioni 50 na kwa sasa una thamani ya Shilingi bilioni 400,” amesema Migangala.
Ameongeza kuwa mifuko ya uwekezaji ya UTT AMIS imeendelea kutoa faida nzuri kwa wawekezaji wake, huku Mfuko wa Umoja ukiwa na faida ya zaidi ya asilimia 12, mingine ikifikia zaidi ya asilimia 13 na 14, na mifuko miwili kuvuka asilimia 15.
“Kwa ujumla, mwaka uliopita ulikuwa mzuri sana kwa uwekezaji,” ameongeza.
Migangala amesema kuwa wakati UTT AMIS inaanza, jumla ya thamani ya mifuko yake ilikuwa Shilingi trilioni 2.2, lakini hadi kufikia mwisho wa mwaka uliopita imeongezeka hadi Shilingi trilioni 3.2, sawa na ongezeko la zaidi ya Shilingi trilioni moja ndani ya mwaka mmoja.
Kwa upande wa idadi ya wawekezaji, amesema taasisi hiyo imepata ongezeko kubwa kutoka wawekezaji takribani laki tatu hapo awali hadi zaidi ya laki tano kwa sasa.
“Tunawashukuru wawekezaji wetu pamoja na Serikali na mamlaka mbalimbali kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, hasa ikizingatiwa kuwa UTT AMIS inafanya kazi ndani ya soko la mitaji,” amesema.
Amesisitiza kuwa bado kuna changamoto ya kuwafikia Watanzania wengi zaidi, lakini jitihada zinaendelea kuzaa matunda.
“Mwanzo hatukuweza kupata hata wawekezaji elfu 10 kwa mwaka, lakini mwaka uliopita pekee tumepata wawekezaji wapya laki moja na elfu hamsini,” amesema Migangala.
Katika kufanikisha hilo, amesema UTT AMIS imeendelea kupanua huduma zake kwa kufungua ofisi mpya mikoani, zikiwemo Morogoro na Kahama mkoani Shinyanga.
Aidha, amesema taasisi hiyo imewekeza katika matumizi ya teknolojia ili kurahisisha uwekezaji kwa wananchi.
“Kwa sasa mifuko yetu inapatikana kupitia mitandao yote ya simu nchini, na pia tumefungua mfumo wa mtandaoni (portal) unaomruhusu mwekezaji kuwekeza popote alipo mradi awe na intaneti,” amesema.
Awali akizungumza, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa UTT AMIS, Profesa Faustin Kamuzora, amesema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 unahitaji mchango mkubwa wa taasisi za uwekezaji katika masoko ya fedha.
Amesema lengo la kuongeza kipato cha Mtanzania kutoka dola 1,300–1,400 za sasa hadi dola 7,500–8,000 linahitaji ushiriki wa taasisi kama UTT AMIS.
“Taasisi yetu ina jukumu la kuwaelimisha wananchi kuhusu elimu ya fedha. Kwa sasa tuna mifuko saba ya uwekezaji, na baada ya kuboresha mifumo yetu tunajiandaa kuanzisha mazao mengine,” amesema Profesa Kamuzora.
Ameongeza kuwa katika safari ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kutoa elimu na taarifa zitakazochochea uwekezaji katika sekta ya fedha.





Comments