Diwani Kigogo: Ndani ya Siku 100 za Rais Samia, Miradi ya Afya, Elimu na Miundombinu Yaendelea Kutekelezwa kwa Kasi

 

Diwani Kigogo: Ndani ya Siku 100 za Rais Samia, Miradi ya Afya, Elimu na Miundombinu Yaendelea Kutekelezwa kwa Kasi


Na Mwandishi wetu, Dar es salaam 

Diwani wa Kata ya Kigogo Manispaa ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es salaam Nassibu Limira, amesema kuwa ndani ya siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya Afya, Elimu na Miundombinu.

Ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari katika mahojiano maalumu ofisini kwake, ambapo diwani huyo amebainisha kuwa Serikali wameanza kutoa bima kwa wazee ili wapate matibabu bure kwani serikali inawapenda na kuwajali watu wa umri huo, kutokana na kundi hilo kukumbwa na magonjwa mara kwa mara huku wengine wakikosa uwezo wa kugharamia matibabu.

"Kama Rais Dkt. Samia alivyotoa ahadi yake ya siku mia moja, tayari tumeanza kuona baadhi ya mambo aliyoahidi yameanza kutekelezwa kwa kasi kubwa sana katika upande wa sekta ya Afya kwa wazee kupatiwa uhakika wa matibabu bure," amesema diwani huyo.

Changamoto Hospitali ya Kigogo

Aidha, diwani huyo ameendelea kusema kuwa Hospitali ya Kigogo licha ya kutoa huduma nzuri, bado inakabiliwa na ufinyu wa eneo, hali inayosababisha kukosekana kwa eneo la kujenga jengo la kuhifadhia maiti. Ameeleza kuwa walipokea mashine lakini walikosa eneo la kuifunga, hivyo wameilazimika kuigawa katika hospitali nyingine za Serikali huku wakiendelea na jitihada kuhakikisha kituo hicho cha afya kinaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa Kata ya Kigogo na maeneo jirani.

Akizitaja jitihada hizo, Mheshimiwa Diwani Limira amesema ni pamoja na kupeleka wazo hilo katika vikao vya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ili wapewe fedha za kuwalipa fidia wananchi waliozunguka eneo la hospitali wahame, ili kupatikana eneo la kujenga jengo la kuhifadhia maiti na wagonjwa.

Sekta ya Elimu

Kwa upande wa elimu, diwani Limira amebainisha kuwa kuna baadhi ya shule ambazo hazijajengewa ukuta, hivyo inahitajika fedha za kuwalipa wananchi waliozunguka shule hizo ili wahame. Ameeleza kuwa katika uongozi wake atajitahidi kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kutekeleza suala hilo.

Ulinzi na Usalama

Aidha, kuhusu ulinzi na usalama, amesema hali imeendelea kuimarika huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku. Ameeleza kuwa wamekuwa wakisisitiza ulinzi shirikishi na kutoa elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa kuchangia katika ulinzi shirikishi.

"Katika mitaa yetu mitano hali ni shwari, lakini bado tuna changamoto ya ofisi ya Serikali iliyochomwa moto katika vurugu za Oktoba 29, 2025, ambapo tunasubiri Serikali ilete fedha ili ukarabati ufanyike na wananchi waendelee kupatiwa huduma za kiofisi kama kawaida," amesema

Comments