DIWANI NYANTORI AELEZA MAKUBWA YALIYOFANYWA KATA YA MBEZI,AMSHUKURU RAIS DKT SAMIA

 DIWANI NYANTORI AELEZA MAKUBWA YALIYOFANYWA KATA YA MBEZI,AMSHUKURU RAIS DKT SAMIA


Dar es Salaam:

Imeelezwa kuwa Kata ya Mbezi iliyopo katika Halmashauri ya Ubungo, Jijini Dar es Salaam, imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo ujenzi wa vivuko, barabara, ukarabati wa shule 12 pamoja na kukamilika kwa Kituo cha Afya cha Msakuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika kata hiyo, Diwani wa Kata ya Mbezi, Bw. Nyantori Pius, amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kupitia utoaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kipaumbele inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Amesema Serikali imetoa Shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa vivuko, zaidi ya Shilingi milioni 600 kwa ukarabati wa shule 12 na zaidi ya Shilingi bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Msumi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.

Bw. Nyantori ameongeza kuwa kazi inayofanywa na Rais Samia ya kushuka hadi ngazi ya wananchi inasaidia kutatua kero zao kwa vitendo, hususan katika sekta ya miundombinu, hatua ambayo imeboresha upatikanaji wa huduma muhimu ndani ya mitaa mitano ya kata hiyo.

Kuhusu sekta ya afya, amesema zahanati ya Msakuzi tayari imekabidhiwa na kuanza kutoa huduma sambamba na Kituo cha Afya cha Mpiji Magohe ambacho kimepandishwa hadhi kutoka zahanati hadi kituo cha afya.

Katika sekta ya maji, Diwani huyo amesema kata hiyo imenufaika na miradi ya maji licha ya changamoto ya upungufu wa maji unaosababishwa na ukame unaoendelea. Amesema Rais Samia ametoa zaidi ya Shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya mradi wa maji wa Mtaa wa Msumi ambapo ujenzi wake tayari umeanza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi, Louis Bawaziri Hassan Tandala, amesema ndani ya siku 100 za Rais Samia, wananchi wamefaidika na ujenzi wa daraja la Kasambala lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 600, ambalo hapo awali lilikuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi na wanafunzi wakati wa mvua.

Aidha, amesema katika sekta ya elimu, Shule ya Msingi Mbezi imepatiwa zaidi ya Shilingi milioni 45 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya majengo na zaidi ya Shilingi milioni 47 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha walimu.

Hata hivyo, viongozi hao wamebainisha kuwa bado kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la wanafunzi shuleni pamoja na upungufu wa maji katika baadhi ya maeneo, licha ya uwepo wa mifumo ya maji kwa kiwango cha asilimia 99.

Comments