Diwani Sanga Aongoza Zoezi la Upandaji Miti Zahanati Mpya Saranga, Aeleza Mafanikio ya Siku 100 za Rais Samia

 

Diwani Sanga Aongoza Zoezi la Upandaji Miti Zahanati Mpya Saranga, Aeleza Mafanikio ya Siku 100 za Rais Samia






Dar es Salaam – Diwani wa Kata ya Saranga, Manispaa ya Ubungo, Mhandisi John Sanga, leo Januari 28, 2026, ameshirikiana na wananchi wa mitaa mbalimbali ya kata hiyo kupanda miti katika eneo la Zahanati mpya ya Saranga, akiwataka wananchi kuitunza miti hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika zoezi hilo, Diwani Sanga amesema upandaji wa miti ni moja ya jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira na kuhakikisha wananchi wanakuwa katika mazingira bora pindi wanapokwenda kupata huduma katika zahanati hiyo ambayo inatarajiwa kufunguliwa rasmi hivi karibuni.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa zaidi ya Shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo mpya ya Saranga ambayo tayari imekamilika ikiwa na vyumba vya madaktari, wagonjwa, vyoo na maabara, na sasa inasubiri kukamilika kwa eneo la kuchomea taka ili ianze kutoa huduma zake kwa wananchi.

Diwani Sanga amesema zahanati hiyo itawanufaisha moja kwa moja wananchi wa Kata ya Saranga ambao kwa sasa wanapata huduma za afya katika maeneo mengine ikiwemo Kituo cha Afya cha Kimara.

Kuhusu utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia tangu aingie madarakani baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025, Diwani Sanga amesema kata hiyo imepokea Shilingi milioni 380 kwa ajili ya mradi wa maji hususan katika mitaa ya King’ong’o na Ukombozi.




Akifafanua, amesema:

"Kati ya maeneo ambayo wananchi wake walipitia changamoto kubwa ya maji basi ni Kata ya Saranga ni mtaa wa King'ong'o ambapo wananchi wake walikuwa na shida kubwa ya maji ila kupitia fedha alizozitoa Mhe. Rais Dkt. Samia kupitia mradi wa King'ong'o Water Boosting tayari zaidi ya asilimia 75 za wakaazi wa mitaa hiyo wanapata huduma za maji safi na salama."

Aidha amesema kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Kibamba watachimba visima katika mitaa yote tisa ya kata hiyo, na tayari fedha zimetolewa ili kupunguza tatizo la upungufu wa maji.

Katika sekta ya miundombinu ya barabara, Diwani Sanga amesema ndani ya siku 100 za Rais Samia wamepokea fedha kwa ajili ya uboreshaji wa barabara ya kutoka Kimara Suka hadi Golani na Saranga hadi eneo ilipo Zahanati ya Saranga kwa kiwango cha changarawe, na mkandarasi tayari yuko kazini.

Kuhusu suala la ulinzi na usalama katika kata hiyo, Diwani Sanga amesema:

"Kuhusu suala la ulinzi na usalama kwenye Kata yetu pia baada ya wananchi kuchoma moto vituo vya polisi viwili katika vurugu za Oktoba 29, kwa sasa tuna vikundi 36 vya ulinzi shirikishi na tayari nimeungana na wananchi wangu kuhakikisha tunajenga Kituo kikubwa cha Polisi ambacho kitasaidia wananchi hasa wa mitaa ya Saranga na Ukombozi katika kuhakikisha kunakuwepo kwa usalama wa raia na mali zao."

Kuhusu elimu, Diwani Sanga amesema mapokezi ya wanafunzi wa darasa la kwanza na wale wa kidato cha kwanza yamekwenda vyema kutokana na mwitikio wa wazazi.

Ameongeza kuwa:

"Mimi kama kiongozi nitahakikisha shule zote sita za msingi na sekondari mbili za Kata hiyo zinakuwa na ufaulu mzuri wa wanafunzi katika matokeo ya mitihani ya Taifa."

Katika hatua nyingine, Diwani Sanga amesema tayari wameanzisha jukwaa la wanawake ambao watanufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ili kujikwamua kiuchumi.








Comments