MFUMO WA E-UTATUZI,WAZINDULIWA WAZIRI SANGU ASEMA UTALETA MAPINDUZI MAKUBWA YA HAKI

  MFUMO WA E-UTATUZI,WAZINDULIWA WAZIRI SANGU ASEMA UTALETA MAPINDUZI MAKUBWA YA HAKI



DAR ES SALAAM.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, amesema kuwa kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa kidijitali wa usajili wa mashauri ya usuluhishi na uamuzi unaofahamika kama e-Utatuzi kunatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa haki nchini.

Waziri Sangu ameyasema hayo leo Januari 21, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa matumizi ya mfumo huo, akibainisha kuwa e-Utatuzi utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama na usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika ofisi za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Amesema mfumo huo utaongeza uwazi, uwajibikaji na kasi katika ushughulikiaji wa mashauri ya kazi, sambamba na kuchochea upatikanaji wa haki kwa wakati pamoja na kuunga mkono ukuaji wa uchumi wa Taifa. Waziri Sangu ameipongeza CMA kwa kazi kubwa na ya kitaaluma iliyofanikisha kukamilika na kuanza kutumika kwa mfumo wa e-Utatuzi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dkt. Yose Mlyambina, amesema mfumo wa e-Utatuzi ni hatua muhimu katika mapinduzi ya kidijitali kwenye sekta ya haki kazi, kwani utaongeza uwazi, ufanisi na kasi ya utoaji wa haki kwa wadau wote.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha usimikaji wa mfumo huo wa kisasa, akisema kuwa utarahisisha utendaji kazi wa Tume na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya mtandao.

Comments