NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA ATAKA BARAZA LA USHINDANI KUIMARISHA ELIMU KWA UMMA
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA ATAKA BARAZA LA USHINDANI KUIMARISHA ELIMU KWA UMMA
DAR ES SALAAM – Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Denis Londo (Mbunge), ametembelea Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal – FCT) na kulipongeza kwa kazi nzuri ya utoaji haki linayoendelea kuifanya, huku akisisitiza umuhimu wa Baraza hilo kuendelea kutoa elimu kwa wadau wake na umma kwa ujumla ili kufahamika zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Londo alisema Baraza la Ushindani lina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa sera ya ushindani nchini, hususan kupitia usikilizaji wa rufaa na mashauri yanayotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani pamoja na Mamlaka za Udhibiti wa Masoko. Alieleza kuwa utekelezaji huo unachangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga mazingira bora ya biashara, kuvutia uwekezaji na kulinda maslahi ya walaji na washiriki wote wa soko. Hata hivyo, Mhe. Londo alibainisha kuwa, licha ya umuhimu wake, Baraza la Ushindani bado halifahamiki kwa wananchi wengi, hali inayolifanya hitaji kuongeza jitihada za utoaji elimu ya umma kuhusu majukumu na mamlaka yake.
Aidha, alisema kuwa uwepo wa taasisi imara kama Baraza la Ushindani ni nguzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa taifa, hasa katika kudhibiti vitendo vya ukiritimba na ushindani usio wa haki unaoweza kudhoofisha masoko na ukuaji wa uchumi. Aliongeza kuwa, ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni muhimu vyombo vya usimamizi na utoaji haki, ikiwemo Baraza la Ushindani, kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji wa hali ya juu, kwa haki, ufanisi na kwa wakati.
Kwa upande wake, Msajili wa Baraza la Ushindani, Bw. Mbegu Kaskasi, alimshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa ziara hiyo na kumhakikishia kuwa Baraza limejipanga kikamilifu kushughulikia mashauri ya rufaa kwa ufanisi na kutoa maamuzi ya haki yanayozingatia sheria na kutolewa kwa wakati, kwa lengo la kulinda maslahi ya wananchi, wafanyabiashara na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Bw. Kaskasi aliongeza kuwa Baraza linaendelea kuimarisha mifumo yake ya kazi, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali pamoja na kuendeleza utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali, hatua itakayoongeza ufanisi katika utoaji wa haki na kuimarisha ushindani wa soko nchini. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kufuatilia na kuimarisha utendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa lengo la kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao ipasavyo katika kulinda uchumi wa Taifa na kuchochea maendeleo endelevu ya nchi.







Comments