TAASISI YA MWALIMU NYERERE YAJA NA MKUTANO NA WAZEE KUJADILI HALI YA AMANI,UMOJA
TAASISI YA MWALIMU NYERERE YAJA NA MKUTANO NA WAZEE KUJADILI HALI YA AMANI,UMOJA
Dar es Salaam, Januari 19, 2026
Taasisi ya Mwalimu Nyerere imepanga mkutano wa mazungumzo kuhusu Amani, Umoja, Haki na Maendeleo ya Tanzania, utakaofanyika Januari 22, 2026 katika ukumbi wa mkutano wa taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Waryoba Butiku, amesema kuwa mkutano huo unalenga kutoa nafasi kwa wazee kujadili na kutoa maoni kuhusu misingi ya taifa, ili kudumisha Amani, Umoja na maendeleo endelevu ya wananchi.
“Tunawaita wazee hapa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa sababu Mwalimu aliamini katika wazee. Wazee si vyeo, bali ni hekima na busara wanayoleta,” amesema Butiku.
Amesema washiriki wa mkutano huo ni watu wenye hekima na busara kutoka kwenye makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo viongozi wa dini, wasomi, wazee wastaafu, wanawake, vijana, vyama vya siasa, tasnia ya habari na taasisi za kiraia.
Butiku ameongeza kuwa umuhimu wa mkutano huu unatokana na matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025.
“Hali tuliyoiona Oktoba 29 inaonyesha nchi kushindwa kuishi katika misingi ya sheria; kila mtu analia kivyake bila kuelewana, hali ambayo Rais aliona ni lazima kuchunguzwa,” amesema.
Aidha, amesema Rais pia aliwahimiza wazee kuunda jukwaa la uzalendo na maadili, ili kusaidia Taasisi kurithisha na kusambaza maadili ya Mwalimu Nyerere, ikiwemo agenda ya amani na usalama, utu na utaifa, pamoja na maendeleo ya sekta ya kilimo.



Comments