TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI YAONGEZA MUDA KWA KWA TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI ZINAZOKUSANYA NA KUCHAKATA TAARIFA BINAFSI
TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI YAONGEZA MUDA KWA KWA TAASISI ZA UMMA NA BINAFSI ZINAZOKUSANYA NA KUCHAKATA TAARIFA BINAFSI
Na Thadei PrayGod,Dar es salaam
Tume ya ulinzi wa taarifa binafsi (PDPC) iketangaza kuongeza muda wa miezi mitatu kwa taasisi za umma na binafsi zinazofanya Kazi ya kukusanya na kuchakata taarifa binafsi
Kwa mujibu wa tume hiyo, muda wa nyongeza unaanzia Januari 8 hadi Aprili 8, 2026, ukiwa ni fursa ya mwisho kwa taasisi ambazo bado hazijatekeleza kikamilifu matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 21, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema kuwa kipindi hicho cha nyongeza kinatoa nafasi kwa taasisi husika kukamilisha usajili wao kwa hiari kabla ya kuanza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Dkt. Mkilia amesisitiza kuwa nyongeza hiyo haimaanishi kusitishwa kwa utekelezaji wa Sheria, bali ni dirisha la mwisho la hiari kabla ya kuanza utekelezaji mkali wa sheria dhidi ya taasisi zitakazobainika kukaidi matakwa yake.
Ameongeza kuwa baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, PDPC itaanza mara moja ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya, kuhifadhi, kuchakata au kusafirisha taarifa binafsi ndani na nje ya nchi.
Ukaguzi huo utalenga kubaini taasisi zitakazokuwa zinaendesha shughuli hizo bila kuzingatia masharti ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na Kanuni zake.
Aidha, Tume imeonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote, taasisi au kampuni itakayobainika kukiuka Sheria hiyo. Kwa mujibu wa Sheria, adhabu zinazoweza kutolewa ni pamoja na kutozwa faini, kifungo au adhabu zote kwa pamoja, sambamba na kulipa fidia kwa waathirika wa ukiukwaji wa haki ya faragha.
PDPC pia imesisitiza kuwa kuvunja faragha au kutumia taarifa binafsi bila ridhaa ya mhusika, au kinyume na taratibu za kisheria, ni kosa linalomuwajibisha mhusika binafsi bila kujali hadhi au ukubwa wa taasisi husika



Comments