WANAHARAKATI AHMED KOMBO NA YONA WA CHALINZE WAOMBA MICHANGO ILI KUZUNGUKA TANZANIA KUHIMIZA AMANI

 

WANAHARAKATI AHMED KOMBO NA YONA WA CHALINZE WAOMBA MICHANGO ILI KUZUNGUKA TANZANIA KUHIMIZA AMANI




Wanaharakati huru hapa nchini Ahmed Kombo na Joseph Yona maarufu kama Yona wa Chalinze  wamewaomba Watanzania, wafanyabiashara pamoja na Serikali kwa ujumla kuwaunga mkono kwa kuwachangia ili waweze kutekeleza ziara ya kitaifa ya kueneza elimu ya uzalendo, umuhimu wa amani kwa Taifa pamoja na uhamasishaji wa vijana kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana nchini.



Wanaharakati huru hao wameyasema hayo walipokuwa Wakizungumza na waandishi wa habari Leo Januari 7,2026 jijini Dar es salaam huku wakisisitiza kuwa  lengo kuu la ziara hiyo ni kuzungumza na Watanzania, hususan vijana, juu ya dhana ya uzalendo wa kweli na wajibu wa kila raia katika kulinda na kudumisha amani ya nchi, wakisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa mshikamano na maendeleo endelevu ya Taifa.

"Yaliyotokea Oktoba 29 hatutaki yajirudie tena nawasihi vijana tutunze amani ya nchi yetu Kuna watu wanadhani tumelipwa ili kufanya haya laa,ndiyo maana tumekuja kuomba michango ya wadau mbalimbali wakiwemo wananchi na wafanyabiashara"alisema mwanaharakati Ahmed Kombo

 Aidha, wameeleza kuwa kupitia ziara hiyo wanatarajia kuwafikia zaidi ya vijana 5,000 katika mikoa mbalimbali nchini kupitia mikutano, mijadala na mazungumzo ya wazi yatakayolenga kuwajengea vijana uelewa mpana juu ya masuala ya uzalendo, amani na matumizi sahihi ya fursa zilizopo kwa maendeleo binafsi na ya Taifa kwa ujumla.

Amesema ziara hiyo itahusisha zaidi ya vijana 300 Kila Mkoa ambao watakaopita huku wakiambatana na waandishi zaidi ya 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

 Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika katika mikoa 15, ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha pamoja na mikoa mingine, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kujenga kizazi chenye uzalendo wa dhati. Kutokana na hilo, Ahmed Kombo na Joseph Yona wamewaomba Watanzania wote wenye mapenzi mema na Taifa kujitokeza kuwaunga mkono kwa kuchangia ili kufanikisha safari hiyo ya kitaifa.

Hata hivyo wanaharakati hao wamesema kuwa akaunti ambayo wanatumia kuomba michango hiyo ni akaunti namba 25510065664 yenye jina la Joseph & Ahmed kupitia NMB

Comments