ACT WAZALENDO KUTOADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI,KUJA NA HILI
Ngome ya wanawake wa Chama cha ACT Wazalendo imetangaza maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani itakayofanyika Machi 8, 2026, kwamba wataiadhimisha kwa kuwakumbuka wananchi waliouawa Oktoba 29, 2025 wakitumia kauli mbiu ya “Machozi ya Mama – Deni la Taifa”.
Oktoba 29, 2025 katika baadhi ya mikoa ikiwamo ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Iringa na Njombe na Dodoma, yalifanyika maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu, yaliyokabiliwa na nguvu ya majeshi ya ulinzi na usalama na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 26, 2026, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa ACT Wazalendo, Janeth Rithe amesema Machi 8 haitakuwa sherehe kwao, bali watakuwa wakiomboleza.
“Mioyo yetu bado inavuja damu. Macho yetu bado yana kiza. Tarehe 29 Oktoba 2025 imeacha kovu lisilofutika katika historia ya maisha yetu. Siku ile, hatukupoteza kura tu; tulipoteza sehemu ya miili yetu.
Amesema kutokana na ukatili uliofanyika, wanawake wa Tanzania wanajiona kuwa kama mkimbizi na kuishi kwa hofu na uoga wasijue litakalowapata kesho ndani ya nchi yao mwenyewe.
“Imani imetoweka, tumaini limevunjika, na demokrasia yetu imezikwa katika kaburi la sahau. Ndiyo maana, mwaka huu, kauli mbiu yetu ni fupi lakini yenye uzito wa mlima: Machozi Ya Mama – Deni La Taifa.
“Machozi yanayotiririka kwenye vilindi vya mioyo ya wajane wa Oktoba 29 ni deni ambalo taifa hili lazima lilipe. Damu ya vijana wetu iliyomwagika barabarani na vichochoroni ni kilio kinachoitafuta haki usiku na mchana. Hatuwezi kuvaa sare za sherehe wakati bado tunavaa nguo za maombolezo,” amesema.
Amesema watautumia mwezi mzima wa Machi 2026 kuwa mwezi wa maombolezo na kumbukumbu ya Kitaifa kwa kutocheza muziki wala kufanya karamu.
Badala yake amesema watafanya ibada na Maombi ya Kitaifa (Selous), ambapo watajumuika Mkoa wa Kichama Selous kuliombea Taifa.
“Tutawaombea marehemu wote wapumzike kwa amani, na kuwaombea majeruhi ambao bado wanaugua maumivu ya miili na roho, ili Mungu awarejeshee afya zao,: amesema.
Amesema pia watatembelea Wazee, kufariji yatima, kufanya huduma za afya na usafi, kuchangia Damu, kuzuru kamilia na kakaburi na kufanya mikutano ya Kushukuru wananchi.
Chanzo:jamii forums



Comments