Diwani Manyinya Azindua Kituo cha maegesho ya Bodaboda Kivule, Atoa Onyo Kali kwa 'wanaoichukulia poa' Kazi hiyo

 

Diwani Manyinya Azindua Kituo cha maegesho ya Bodaboda Kivule, Atoa Onyo Kali kwa 'wanaoichukulia poa' Kazi hiyo


Na Mwandishi wetu, Dar es salaam 

DIWANI wa Kata ya Kivule Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam CPA Rajab Manyinya amewataka maafisa usafirishaji wa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda wa kata hiyo kuheshimu kazi hiyo kwani inawaingizia kipato cha kuendesha maisha yao na kuhudumia familia.

Diwani Manyinya ameyasema hayo alipokuwa akizindua kituo cha maegesho ya bodaboda kilichopo katika mtaa wa Kerezange, Kanyigo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoahidi kwa maafisa usafirishaji hao wakati akiomba kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana.

Amesema ni marufuku kwa madereva wa kituo hicho kutumia dawa za kulevya ikiwemo bangi na vilevi na badala yake wafanye kazi zao kwa bidii ili kuendelea kupata wateja ambao watawaamini.


"Kuna bodaboda nawafahamu katika eneo hili la Kivule amejenga nyumba kwa kuendesha bodaboda na mpaka mke akao hivyo na nyie msione kama kazi hii ni kazi ya wahuni na nitawaletea afisa kutoka Halmashauri hapa asajili kituo chenu na kuwapa vitambulisho rasmi mtambulike kisheria" amesema.

Diwani Manyinya amesema wakati anaomba kura kwa kuzunguka nyumba kwa nyumba mtaa kwa mtaa, alikutana na kero ya kukosekana kwa maegesho ya bodaboda hasa kipindi cha mvua na jua hivyo ndani ya siku 100 amefanikisha ujenzi wa kituo hicho.

Amewataka bodaboda hao kuvaa vizuri ili kuwavutia wateja wanaowapakia katika vyombo vyao vya usafiri huku akiahidi kuwawekea televisheni na kisimbuzi katika kituo hicho ili kukiboresha zaidi.

"Nimeanza kwa vitendo kwa kushughulikia changamoto mbalimbali za wakaazi ya kata hii ikiwemo ujenzi wa barabara ya kwa Mkolemba hadi Miembeni na maeneo mengine ya Bombambili na Magole na bodaboda nao watanufaika na miundombinu hiyo katika kutoa huduma ya usafirishaji" amesema.


Amesema kuwa ameweka msisitizo kwa kuhakikisha anaboresha miundombinu ya barabara za kata hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara inayotoka Msongola kuelekea eneo la Sirari kwa kiwango cha lami ambapo tayari mkandarasi yuko saiti na ujenzi umeshaanza.

Hata hivyo ameongeza kuwa kwa upande wa afya amesimamia kuanzishwa kwa chuo cha uuguzi ndani ya kata hiyo katika eneo la hospitali ya Kivule ambapo shilingi milioni 900 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo hivyo pia atahamasisha vyuo vingine kufungua kampasi katika Kata ya Kivule.

Katika hatua nyingine diwani huyo amewahamasisha wakaazi wa mitaa ya kata hiyo kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwa wote ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya bila kutumia fedha taslimu (cash) ambapo pia watapunguza gharama za huduma za matibabu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiwe cha bodaboda Kanyigo Sylvester Cleofasi amemshukuru diwani kwa kujengwa kwa kituo hicho na kuahidi kukitunza vyema huku akiwataka bodaboda wenzake kuwa waaminifu wanapopakia abiria.

Ameomba Serikali kuangalia namna ya kukomesha changamoto ya bodaboda za mikatana kwani inawakabili vijana wengi ambao wanaingia mikataba isiyoeleweka ikiwemo wale wanaokopa pikipiki.

Amesisitiza kuwa dhumuni la kituo, kituo kisajiliwe na kutambulika kisheria ili kuepisha vitendo vya uhalifu.



Comments