JIJI LA DAR ES SALAAM LAJIVINIA KUTEKELEZA ZAIDI YA ASILIMIA 89 YA MIRADI YA MAENDELEO, BILIONI 1 YAWEKEZWA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA

 JIJI LA DAR ES SALAAM LAJIVINIA KUTEKELEZA ZAIDI YA ASILIMIA 89 YA MIRADI YA MAENDELEO, BILIONI 1 YAWEKEZWA  UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA




Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekamilisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa zaidi ya asilimia 89, hatua inayodhihirisha kasi ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Ilala.


Akizungumza leo Februari 25, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Mpogolo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuunga mkono na kusukuma mbele miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi.


Mpogolo alieleza kuwa Wilaya ya Ilala ina zaidi ya watoto 400,000 wanaosoma katika shule za msingi na sekondari, hali inayosababisha changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati. Alisema Halmashauri imejikita kuongeza miundombinu ya elimu ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia.


Kwa mujibu wa Mpogolo, Halmashauri imetenga Shilingi milioni 400 kwa elimu ya msingi na Shilingi milioni 400 kwa shule za sekondari, ambapo kwa sasa wakandarasi wako katika hatua za kutengeneza madawati ili kupunguza uhaba uliopo mashuleni.


Aidha, alisema katika bajeti ya mwaka 2026/2027, Halmashauri imetenga Shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa vyumba, hatua inayolenga kukabiliana na ongezeko la wanafunzi na kuboresha ubora wa elimu.


Katika hatua nyingine, Mstahiki Meya wa Jiji la Ilala, Nurdin Bilal, aliwaomba wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kushiriki mafunzo ya pamoja ya maadili na uongozi bora, ili kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi na kusimamia vyema miradi ya maendeleo.


Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pia imeeleza kuwa inatarajia ifikapo mwaka 2028 idadi ya watoto wanaoanza Kidato cha Kwanza itaongezeka kwa kiasi kikubwa, huku makadirio yakionyesha zaidi ya watoto 65,000 watajiunga na ngazi hiyo, hali inayohitaji maandalizi ya mapema ya miundombinu ya elimu.

Comments