Skip to main content

KAMISHNA KUJI AFANYA ZIARA YA KIKAZI HIFADHI YA TAIFA NYERERE

 

KAMISHNA KUJI AFANYA ZIARA YA KIKAZI HIFADHI YA TAIFA NYERERE




NA MWANDISHI WETU

Kamishna wa Uhifadhi  TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji  Februari 08, 2026 amefanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Nyerere na kukagua maendeleo ya shughuli za uhifadhi na utalii sambamba na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika hifadhi hiyo hasa miradi iliyotekelezwa kupitia Mradi wa Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Ziara ya Kamishna Kuji ililenga kufanya ukaguzi wa shughuli za uhifadhi na utalii pamoja na miundombinu inayotumiwa na watalii ambapo katika ukaguzi huo alifika katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Mtemere.

Maeneo mengine aliyokagua ni Lango la kuingilia watalii la Mtemere, Nyumba za watumishi ambazo zitasaidia Maafisa na Askari Uhifadhi kupata makazi pamoja na uwepo wa eneo la kambi za doria, Nyumba za kulala wageni (Rest House) na Kambi ya kulala watalii (Campsite).

Kamishan Kuji aliwapongeza Maafisa na Askari kwa kusimamia shughuli zote za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya hifadhi hiyo kulikopelekea miradi hiyo kukamilika kwa ufanisi mkubwa. 

Ukamilishwaji wa miradi hiyo unaenda kuleta mapinduzi makubwa katika ongezeko la watalii na mapato kwa Taifa pamoja na kuvutia idadi kubwa ya watalii na wawekezaji.

Katika ziara hiyo, Kamishna Kuji alipokelewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi John Nyamhanga - Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo - Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere. 

Kamishna Kuji aliambatana na viongozi wengine wa Shirika wakiwemo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Izumbe Msindai - Mkuu wa Kanda ya Magharibi na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara.

Comments