Kampuni ya GF Trucks & Equipment LTD Kudhamini Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Singida Black Stars

 

Kampuni ya GF Trucks & Equipment LTD  Kudhamini Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Singida Black Stars



Na Thadei PrayGod 

Dar es Salaam, Februari 13, 2026 – Kampuni ya GF Trucks & Equipment LTD imeingia makubaliano rasmi ya kudhamini tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi (Player of the Month) kwa klabu ya Singida Black Stars FC, katika hatua inayolenga kukuza na kuendeleza sekta ya michezo nchini.

Akizungumza katika hafla ya utilianaji Saini wa makubaliano hayo  iliyofanyika makao makuu ya kampuni hiyo yaliyoko Vingunguti Jijini Dar es salaam,Mkurugenzi wa Masoko na Biashara wa kampuni hiyo, Bw. Salman Karmali, alisema udhamini huo ni sehemu ya mchango wa kampuni katika kusaidia maendeleo ya michezo sambamba na shughuli zake za biashara.

Alieleza kuwa kampuni hiyo imekuwepo kwa miaka 19 na imekuwa mdau mkubwa katika sekta ya malori na mitambo nchini Tanzania, huku pia ikishiriki katika shughuli za kijamii (CSR) ikiwemo michezo, afya na miundombinu.

“Kupitia udhamini huu wa Mchezaji Bora wa Mwezi, tunalenga kuleta chachu kwa vijana, kuhamasisha afya na ushindani katika michezo, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya michezo,” alisema Karmali.

GF pia iliipongeza Singida Black Stars FC kwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, jambo linaloashiria kukua kwa sekta ya michezo nchini.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo, huku ikisisitiza mchango wake katika sekta ya ujenzi na miundombinu kupitia bidhaa zake ikiwemo magari makubwa ya FAW na mitambo ya XCMG kama excavator na wheel loader, ambayo pia inaweza kutumika katika ujenzi wa viwanja vya michezo.

Aidha, GF imetoa pongezi kwa uongozi wa Singida Black Stars, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Serikali kwa kuendelea kukuza sekta ya michezo nchini.

Makubaliano hayo yanatajwa kuwa mwanzo wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya GF Trucks & Equipment LTD na Singida Black Stars FC.

Kwa upande wake uongozi wa Singida Black Stars umeelezea makubaliano hayo kama ishara ya kutoa morali kwa wachezaji wa timu hiyo kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ambayo klabu inashiriki katika ligi kuu ya Tanzania bara.

Comments