MAONESHO YA ADORABLE WEDDING TRADE FAIR 2026 KUFANYIKA APRILI 17–19 EACLC UBUNGO
MAONESHO YA ADORABLE WEDDING TRADE 2025 FAIR KUFANYIKA APRILI 17–19 EACLC UBUNGO
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM – Mkurugenzi Mtendaji wa Adorable Wedding Trade Fair, Anna Lema , ametangaza kufanyika kwa maonesho maalum ya biashara yanayowakutanisha watoa huduma mbalimbali za sherehe na harusi kuanzia Aprili 17 hadi 19 mwaka huu.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Anna amesema maonesho hayo yataleta pamoja watoa huduma wa sekta ya harusi ikiwemo waandaaji wa shela za harusi, watengenezaji wa keki, wabunifu wa mavazi ya harusi na huduma nyingine zinazohusiana na maandalizi ya sherehe.
Amesema maonesho hayo yatafanyika katika soko la kimataifa la Afrika Mashariki EACLC lililopo Ubungo jijini Dar es salaam
Amesema katika maboresho ya mwaka huu, watoa huduma watatumia fremu za maduka zilizopo ndani ya jengo husika kama mabanda ya kuoneshea bidhaa na huduma zao, hatua ambayo imepunguza gharama za maandalizi ukilinganisha na awali ambapo walilazimika kukodisha mabanda kwa gharama kubwa.
Kwa mujibu wa Anna, gharama kwa watoa huduma kushiriki maonesho hayo zitakuwa kati ya Shilingi laki moja na nusu hadi laki nne, kulingana na ukubwa na aina ya nafasi watakayochagua.
Aidha, washiriki watapata fursa ya kuonesha hatua zote za maandalizi ya bidhaa zao, kuanzia mwanzo hadi mwisho, ikiwemo utengenezaji wa shela za harusi na mapambo ya keki, jambo linalotarajiwa kuwapa wananchi uelewa mpana kuhusu ubora na ubunifu uliopo katika sekta hiyo.
Maonesho hayo pia yatakuwa na jukwaa maalum kwa ajili ya kuonesha mavazi ya harusi (fashion show), ambapo wabunifu mbalimbali watapata nafasi ya kutangaza kazi zao mbele ya hadhira.
Kwa upande wa mahudhurio, wananchi wataingia bila kulipa kiingilio chochote katika siku zote za maonesho, hatua inayolenga kuwapa Watanzania wengi zaidi fursa ya kushuhudia bidhaa na huduma mbalimbali za harusi.
Wakizungumzia udhamini wa tukio hilo, mwakilishi wa East African Business Council (EABC) amesema wameamua kudhamini maonesho hayo kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za kukuza biashara za ndani na kutoa fursa kwa Watanzania kujionea bidhaa za sherehe za harusi bila malipo, sambamba na kuwasaidia watoa huduma kujitangaza na kupanua wigo wa soko lao.
Maonesho ya Adorable Wedding Trade Fair yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wabunifu, wafanyabiashara na wananchi katika sekta ya harusi nchini.
- Get link
- X
- Other Apps




Comments