MARUFUKU MICHANGO HOLELA KWENYE SHULE ZA KATA YANGU: DIWANI MUSHI
MARUFUKU MICHANGO HOLELA KWENYE SHULE ZA KATA YANGU: DIWANI MUSHI
KIPUNGUNI, DAR ES SALAAM – Diwani wa Kata ya Kipunguni,Halmashauri ya ya jiji la Dar es salaam, Steven William Mushi, amepiga marufuku mara moja michango yote holela katika shule za kata hiyo, akisema hakuna mzazi au mlezi atakayechangishwa fedha bila kibali cha wilaya, kufuatia ziara yake ya ukaguzi katika shule za Msingi Kipunguni, Kilimani na Sekondari ya Kipunguni.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Diwani Mushi amesema hatua hiyo imelenga kulinda wazazi dhidi ya michango isiyo rasmi na kuhakikisha uwazi katika uendeshaji wa masuala ya elimu. Amesema michango yote iliyobainika ilikuwa ikifanyika bila kufuata taratibu, hali iliyomlazimu kutoa maelekezo ya kusitishwa mara moja hadi kibali halali kitakapopatikana.
Katika ziara hiyo, Diwani Mushi amebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo utoro sugu wa wanafunzi, utukutu, upungufu wa madawati pamoja na changamoto za lishe shuleni, akisema hali hiyo inachangia kushuka kwa ufaulu endapo haitadhibitiwa mapema.
Kutokana na hali hiyo, amesema kuna umuhimu wa kuweka mkakati madhubuti wa kudhibiti utoro, ambapo kila siku majina yanapoitwa shuleni, walimu wanapaswa kuorodhesha wanafunzi wasiohudhuria masomo. Amesema wanafunzi watoro sugu wataandikiwa barua za wito kwa wazazi wao kuitwa shuleni, na wazazi watakaogoma kuitikia wito huo, majina yao yatawasilishwa katika ofisi ya kata kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.
“Nahitaji kuona ufaulu unaongezeka. Hilo haliwezi kufikiwa bila kuhakikisha kila mtoto anakuwepo shuleni na mzazi anatimiza wajibu wake,” amesema Diwani Mushi.
Aidha, ametoa maelekezo kwa uongozi wa shule kuwasilisha ripoti za mahudhurio ya wanafunzi na watoro sugu kila siku ya Ijumaa katika ofisi yake, sambamba na kuwasilisha taarifa zote muhimu ikiwemo changamoto za shule ili ufumbuzi upatikane kwa haraka.
Kuhusu suala la lishe shuleni, Diwani Mushi amesema chakula kwa wanafunzi ni jambo la msingi, lakini amesisitiza kuwepo kwa tathmini ya kina ili kubaini gharama halisi za chakula na kuzitenganisha kwa uhalisia, badala ya wazazi kuchangishwa fedha kwa makadirio yasiyoendana na uhalisia wa gharama.
Amewasihi wazazi na walezi wa Kata ya Kipunguni kushirikiana kikamilifu na walimu pamoja na viongozi wa serikali, akisisitiza kuwa maendeleo ya mwanafunzi yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya mzazi, walimu na viongozi. Amesema kuitikia wito wa mikutano ya shule ni jambo la lazima kwa mzazi anayejali maendeleo ya mtoto wake.
Akizungumzia utekelezaji wa siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Diwani Mushi amesema kata ya Kipunguni tayari imezindua jengo jipya la ghorofa nne lenye madarasa 20, vyoo 40 pamoja na lifti, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya elimu na mazingira ya kujifunzia.
Amehitimisha kwa kusema kuwa ofisi ya kata itaendelea kushirikiana na wazazi, walimu pamoja na viongozi wa serikali kuhakikisha changamoto zote zilizobainika katika ziara hiyo zinapatiwa ufumbuzi wa haraka kwa manufaa ya wanafunzi wa Kata ya Kipunguni.







Comments