TMA YATANGAZA MWELEKEO WA MVUA ZA MASIKA NCHINI,YATOA TAHADHARI HIZI
TMA YATANGAZA MWELEKEO WA MVUA ZA MASIKA NCHINI,YATOA TAHADHARI HIZI
Mamlaka ya Hali ya Hewa hapa nchini (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2026 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka kwa kipindi Cha Mwezi Machi Hadi Mei 2026 huku mamlaka hiyo ikitoa tahadhari katika sekta mbalimbali.
Akitangaza msimu wa mvua hizo mbele ya waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini,leo Februari 5,2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi Dkt. Ladislaus Chan’ga alisema maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
“Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi ikihusisha Pwani ya Kaskazini pamoja na baadhi ya maeneo ya Magharibi mwa ukanda wa Ziwa Viktoria (mikoa ya Kagera na Geita) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, isipokuwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria (mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu) mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa”. Alisema Dkt. Chang’a.
Katika taarifa hiyo ilielezea kuwa Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari na ya kwanza ya mwezi Machi , 2026 katika maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria; na wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi katika maeneo ya pwani ya kaskazini; na wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi, 2026 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, Mvua hizo zikitarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei na wiki ya kwanza ya mwezi Juni 2026 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka huku ongezeko la mvua likitarajiwa katika kipindi cha mwezi Aprili 2026.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao katika baadhi ya maeneo, hususan yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani. Kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kinatarajiwa kupungua hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji, hivyo kushauri watumiaji wa tarifa hizo kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta zao.
Angalizo la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa lilitolewa hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastan huku watumiaji wa taarifa hiyo wakishauriwa kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
- Get link
- X
- Other Apps





Comments