TRA yasisitiza umuhimu wa Waendeshaji wa Bandari kavu (ICDS) Kutokwepa Kodi

 

TRA yasisitiza umuhimu wa Wamiliki wa Bandari kavu (ICDS)  Kutokwepa Kodi



Na Thadei PrayGod, 
Dar es Salaam

Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, amewataka wamiliki na waendeshaji wa bandari kavu nchini  kuachana na tabia ya ukwepaji kodi na kuzingatia masharti ya kisheria ili kurahisisha shughuli za kibiashara.

Akizungumza leo, Februari 19, jijini Dar es Salaam,na waendeshaji wa bandari hizo Kamishna Mwenda alisema TRA ina mpango wa kufanya kazi masaa 24 ili kuongeza ufanisi wa bandari na biashara nchini.

"Leo tumekuja kuwasikiliza wanakikundi cha wamiliki wa bandari kavu ni nini kinakwamisha. Tumepata taarifa kuwa baadhi ya maeneo kuna upungufu wa taa, na tutaweka mfumo ili kuleta ufanisi zaidi," alisema Kamishna Mwenda.

Aliongeza kuwa TRA itaendelea kufanya uchunguzi juu ya ucheleweshaji wa uondokaji wa baadhi ya makontena, huku akisisitiza kwamba baadhi ya ICD zinapokea mizigo zaidi ya uwezo wake.


"Ni lazima tuzisaidie ICD kuwa na usalama wa kutosha, na pia tuongeze ufanisi hususan kupitia uboreshaji wa mifumo," alisema Mwenda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Angelina Mgalula, alisema kuwa sekta ya usafirishaji ni mojawapo ya sekta tano zinazotarajiwa kuleta mapinduzi ya kiuchumi. Aliongeza kuwa wadau wa kibiashara wanapaswa kuwa na mikakati madhubuti ya kukuza pato la taifa.
"Sekta ya usafirishaji na uchukuzi inatarajiwa kuleta mapinduzi ya mapato ya serikali kutoka dola 85 bilioni hadi kufikia dola trilioni moja," alisema Mgalula.

Aidha, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Bandari Kavu, Medard Shangwe, ambaye anawakilisha wanachama wapatao 80, alimpongeza TRA kwa kuwa na mifumo mizuri katika bandari.

"Tunaomba ukaguzi uendelee kadri makontena yanavyoingia ili kuhakikisha shughuli zinaendelea kwa ufanisi," alisema Shangwe.

Comments