Fainali za Kabwili Cup 2026 Kutikisa Dar , Bingwa Kuzawadiwa Gari Alhamis hii
Fainali za Kabwili Cup 2026 Kutikisa Dar , Bingwa Kuzawadiwa Gari Alhamis hii
Mchezo wa fainali za mashindano ya Kabwili Cup 2026 zinatarajiwa kufanyika Alhamis March 19,2026 kuanzia saa 2 usiku katika Uwanja wa Tabata Twiga, huku zawadi nono zikisubiri washindi wa michuano hiyo inayozidi kujizolea umaarufu mitaani.
Fainali hiyo itawakutanisha timu za Makuburi SC dhidi ya timu ya Azimio FC zenye maskani yake mitaa ya Tabata
Akizungumza kuelekea tamati ya mashindano hayo, mratibu wa Kabwili Cup ambaye ni mchezaji wa zamani wa Klabu ya Young Africa Sports Club (Yanga),Ramadhan Kabwili amesema kuwa timu itakayonyakua ubingwa itazawadiwa gari, ikiwa ni moja ya zawadi kubwa kuwahi kutolewa katika michuano ya mtaani.
Aidha Kabwili amesema kuwa kutakuwa na utoaji wa tuzo mbalimbali kwa wachezaji waliofanya vizuri katika vipengele tofauti huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye fainali hizo.
Kabwili amesisitiza wakazi wa eneo la Twiga,Tabata kuzitunza taa zilizowekwa uwanjani hapo na mdhamini ambaye ni kampuni ya Nanasi Group, ili ziweze kudumu na kuendelea kusaidia maendeleo ya michezo katika jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nanasi Group, kampuni inayojihusisha na usafirishaji na uagizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi, alithibitisha kudhamini maboresho ya uwanja huo kwa kuweka taa za kisasa, ili kuruhusu michezo kufanyika usiku.
Pia aliahidi kuendelea kushirikiana katika siku ya fainali kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa mafanikio makubwa ambapo atatoa zawadi ya gari kwa timu itakayonyakua ubingwa wa Michuano hiyo.
Katika kuhakikisha ushindani wa hali ya juu, waamuzi wenye beji za FIFA wanatarajiwa kuchezesha fainali hiyo, jambo litakaloongeza hadhi ya michuano hiyo inayofanyika kwa mwaka wa sita sasa.
Kabwili alisisitiza kuwa mashindano hayo yanalenga kukuza vipaji vya vijana, akibainisha kuwa vipaji vingi vya mpira wa miguu vinatoka maeneo ya uswahilini, na yeye mwenyewe ni zao la mazingira hayo. Aliwataka vijana wenye vipaji kutokata tamaa na kuendelea kujituma ili kufikia ndoto zao.
Ratiba ya siku ya fainali inaonesha kuwa kutakuwa na michezo ya watoto chini ya umri wa miaka 11 itakayoanza saa 11 jioni, huku mechi ya wakubwa ikipigwa kuanzia saa 2 usiku,ikiwakutanisha Makuburi SC na Azimio SC ambapo wadau na mashabiki wanatarajiwa kukesha viwanjani kushuhudia burudani hiyo ya kipekee.
Kocha wa timu ya Makuburi SC amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia fainali hizo, akieleza kuwa ni fursa muhimu kwa jamii kuunga mkono maendeleo ya soka la vijana.
Naye Kapteni wa timu ya Azimio, Seseme, ameahidi ushindi katika mchezo huo wa fainali, huku akimpongeza Kabwili kwa kuandaa mashindano hayo kwa miaka sita mfululizo. Pia alieleza kufurahishwa na uwekaji wa taa uwanjani hapo na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kudhamini michezo ya aina hiyo kwa maendeleo ya soka la nchini.
- Get link
- X
- Other Apps



Comments