MKUTANO WA TANZANIA NA UGANDA KUIMARISHA USHIRIKIANO WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM

  MKUTANO WA TANZANIA NA UGANDA KUIMARISHA USHIRIKIANO WAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM



Dar es Salaam leo imekuwa mwenyeji wa mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja (Joint Permanent Commission - JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda, mkutano unaolenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili jirani.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo, ambaye amesisitiza umuhimu wa jukwaa hilo kama sehemu muhimu ya kuimarisha mahusiano ya pande mbili pamoja na kupanua ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Balozi Shelukindo amesema kuwa Tume ya Kudumu ya Pamoja inatoa fursa muhimu kwa nchi hizo mbili kufanya mazungumzo yenye kujenga, kupitia maendeleo ya ushirikiano uliopo, pamoja na kubaini maeneo mapya ya ushirikiano yatakayowanufaisha wananchi wa Tanzania na Uganda.

Aidha, mkutano huo unawakutanisha maafisa waandamizi wa serikali kutoka Tanzania na Uganda kwa lengo la kupitia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita ya JPC pamoja na kujadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, miundombinu, nishati na usafirishaji.

Vilevile, majadiliano yanatarajiwa kujikita katika kutafuta suluhu za changamoto zinazoweza kuathiri biashara ya mipakani kati ya nchi hizo mbili, ikiwemo kuondoa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru ili kurahisisha biashara na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania na Uganda.

Comments