RAIS SAMIA KUZINDUA MATANKO 15 YA MAFUTA DAR KESHO, WANANCHI WAITWA
RAIS SAMIA KUZINDUA MATANKO 15 YA MAFUTA DAR KESHO, WANANCHI WAITWA
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema kuwa Machi 3, 2026, katika Bandari ya Dar es Salaam, kutafanyika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa matenki 15 ya kuhifadhia mafuta. Hafla hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali wa kupanua na kuboresha bandari hiyo kama lango kuu la biashara nchini.
Akizungumza leo Machi 2, 2026, Mbarawa amesema mgeni rasmi katika tukio hilo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambaye ataongoza hafla hiyo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya uchukuzi na uchumi wa taifa.
Hata hivyo Prof. Mbarawa ameeleza kuwa ujenzi wa matenki hayo utaongeza uwezo wa taifa katika kuhifadhi mafuta na kuboresha mnyororo wa usambazaji wa nishati, hatua itakayochochea biashara za ndani na za kimataifa kupitia bandari hiyo.
“Mradi huu unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya nchi,” amesema Mbarawa.
Mradi huo ni sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, yakilenga kuongeza ufanisi wa huduma, kuvutia uwekezaji na kuiweka Tanzania katika nafasi bora kama kitovu cha biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki.









Comments