SIKU YA USALAMA NA AFYA KAZINI APRILI 28 KUANGAZIA USTAWI WA WAFANYAKAZI
SIKU YA USALAMA NA AFYA KAZINI APRILI 28 KUANGAZIA USTAWI WA WAFANYAKAZI
Serikali imesema maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani mwaka huu yataweka mkazo katika afya ya akili kazini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokana na shughuli za kikazi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini), Deus Clement Sangu, amesema lengo ni kuongeza uelewa na kuhamasisha uboreshaji wa mazingira ya kazi nchini.
Amesema maadhimisho hayo yalianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2004 na kwa mwaka huu yatafanyika kitaifa mkoani Njombe, yakiratibiwa na Serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na wadau wa utatu ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kauli mbiu ya mwaka huu ni “Mazingira Bora ya Kazi Kisaikolojia ni Njia ya Kuimarisha Ustawi wa Wafanyakazi na Kujenga Taasisi Imara,” ikiwa inalenga kuhimiza umuhimu wa afya ya akili kazini kama sehemu muhimu ya kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji.
Ameeleza kuwa vihatarishi vya kisaikolojia vinavyotokana na namna kazi inavyobuniwa, kusimamiwa na mazingira ya kijamii kazini vina athari kubwa kwa afya ya wafanyakazi, na vinaweza kusababisha msongo wa mawazo, kupungua kwa ufanisi pamoja na ongezeko la ajali mahali pa kazi.
Akinukuu takwimu za kimataifa, amesema zaidi ya wafanyakazi milioni 760 duniani wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili zinazohusiana na kazi, hali inayosababisha upotevu mkubwa wa tija na hasara za kiuchumi zinazokadiriwa kufikia zaidi ya dola trilioni moja kila mwaka.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Sangu amesisitiza umuhimu wa waajiri kuhakikisha wanaboresha mazingira ya kazi kwa kuzingatia ustawi wa wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kupunguza mzigo mkubwa wa kazi, kuboresha mahusiano kazini na kuhakikisha usalama wa ajira.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zitasaidia kulinda nguvu kazi ya taifa, kuongeza tija katika uzalishaji na kujenga taasisi imara zinazoweza kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Aprili 28, 2026, mkoani Njombe.



Comments