TANZANIA NI NCHI TAJIRI WAZEE WETU WALITUACHIA RASILIMALI TUZITUMIE VIZURI:SHIGONGO

 



Mbunge wa Jimbo la Buchosa,Mkoani Mwanza Erick Shigongo amesema rasilimali zilizopo kwa sasa nchini ni matokeo ya viongozi walikuwepo awali ambao walizitunza ili vizazi vilivyopo na vijavyo vije kunufaika.



Shigongo ameyasema hayo hii Leo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari kando ya mkutano wa uzinduzi wa jukwaa la uzinduzi wa vijana  lililoandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam.

Amesema Tanzania ni nchi tajiri mno na atalizungumza hilo mara nyingi na Kila siku hatoacha kusifu utajiri wa rasilimali zilizopo nchini.

"wazee wetu Hawa walijua kuwa chini ya ardhi Kuna uranium,tena wakiwa vijana wakati ule walijua pia chini Kuna almasi,tanzanite,dhahabau na gesi na wakajua chini Kuna utajiri mkubwa ila baada ya uhuru lakini wakasema hatutautumia utajiri huu sisi watakuja wautumie watoto wetu" amesema Shigongo.

Ameongeza kuwa Kazi ya viongozi wa wakati huo Ilikuwa ni moja tu kumuondoa mkoloni na walipofanikiwa kumuondoa nao wakafanya Kazi kwa muda na walipozeeka wakaondoka na kuwaachia uongozi vijana ambao wengi walikuwa ni watoto wakati nchi inapata uhuru,hivyo Kazi ya vijana sasa ni kulitoa Taifa hapa lilipo kwa kutumia rasilimali zilizopo.

"sisi Kazi yetu ni kuzitumia sasa rasilimali hizi kupeleka Taifa mbele dhidi ya maadui ujinga,maradhi na umasikini,kwa utajiri huu uliopo kama wazee wale wangekuwa na tamaa wangesema tumepata uhuru sasa tugawane na wangechukua Kila kitu,lakini kwa moyo wa uzalendo wa kupenda Taifa,hawakugusa wakatuachia sisi" amesisitiza Shigongo.

Aidha ameongeza kuwa vijana waliopo sasa wanapaswa kutumia utajiri wa rasilimali uliopo nchini kwa ajili ya kuandaa vizazi bora vijavyo ambavyo vitakuta nchi ikiwa kwenye maendeleo makubwa kiuchumi.

Hata hivyo amewataka vijana kutumia uzuri wa Tanzania na rasilimali zake kama alama inayochangia katika utulivu na amani kwa kuitunza amani ya Taifa ili vizazi na vizazi viendelee kurithi mema.

Comments