VIJANA ACT WAZALENDO WASHAURI KUPUNGUZWA KWA KODI ZA MAFUTA ILI KULETA UNAFUU WA MAISHA KWA WATANZANIA
HUKU mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania wakionja adha ya upandaji wa bei kwa bidhaa za mafuta kutokana na mgogoro uliosababisha vita unaoendelea kati ya Marekani, Israel dhidi ya nchi ya Iran jambo ambalo limepelekea wananchi kulalamikia kupanda kwa gharama za maisha nchini, chama cha ACT Wazalendo kupitia ngome ya vijana,kimeishauri serikali kuondoa angalau Shilingi 500 katika kodi na tozo za mafuta kwa kila lita ili kupunguza mzigo unaoendelea kuwaathiri wananchi wa kipato cha chini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ngome ya vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema ongezeko la bei ya mafuta limeendelea kuchochea kupanda kwa nauli za usafiri, bei za vyakula na huduma nyingine muhimu huku wananchi wengi wakishindwa kuhimili hali hiyo.
Amesema kwa sasa jumla ya kodi na tozo katika lita moja ya petroli na dizeli zimefikia zaidi ya Sh. 1,100, hali ambayo imechangia bei ya mafuta kuendelea kuwa juu katika soko la ndani licha ya malalamiko ya wananchi kuongezeka.
"Kutokana na kupanda kwa gharama hizo tunaiomba serikali iondoe angalau sh. 500 katika kodi na tozo za mafuta kwa kila lita ili kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi na kushusha gharama za bidhaa muhimu,” amesema Nondo.
Mbali na kupunguza tozo, amesema chama hicho pia kinashauri serikali kutoa ruzuku ya mafuta ya angalau Sh. 400 kwa kila lita ili kusaidia kupunguza athari za mfumuko wa bei unaoendelea kujitokeza katika sekta mbalimbali za uchumi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 (The Petroleum Act, 2015), Kifungu cha 166 kinaeleza kuwa bei za mafuta zitasimamiwa kwa mfumo wa soko lakini chini ya usimamizi wa mamlaka husika.
Aidha, Kifungu cha 167 cha sheria hiyo kinna eleza kuwa serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya mafuta kwa kushirikiana na waziri wa fedha wana mamlaka ya kuweka au kurekebisha tozo za mafuta nchini .
Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA), mabadiliko ya bei za mafuta nchini hutokana na bei ya mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji, thamani ya dola ya Marekani pamoja na kodi na tozo za ndani zinazotozwa katika kila lita ya mafuta.
Kuhusu maadhimisho ya miaka 12 ya ACT Wazalendo ngome hiyo ya vijana imepongeza viongozi na wanachama wake kwa maadhimisho ya miaka 12 ya chama hicho yaliyofanyika kitaifa katika Jimbo la Kilwa Kusini Mei 5, 2026, huku kikisema kitaendelea kuisimamia serikali katika masuala ya uchumi na ustawi wa wananchi,huku kikishauri utoaji mikopo wa vijana unaotolewa na wizara ya maendeleo ya vijana kuangaliwa upya.



Comments