JAJI MSHIBE ASISITIZA MAANDALIZI YA KISEKTA KATIKA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO

 JAJI MSHIBE ASISITIZA MAANDALIZI YA KISEKTA KATIKA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO


Dodoma, 14 Agosti 2026: 

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mheshimiwa Jaji Mshibe Ali Bakari, amezitaka sekta zote nchini kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa katika kufanya maandalizi ya kisekta ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na uwepo wa El Niño.

Mhe. Jaji Mshibe aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa 25 wa kujadili Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli, Oktoba hadi Disemba 2026, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa PSSSF, Dodoma.

“Tunapojiandaa kupokea taarifa ya utabiri wa mvua za Vuli, Oktoba hadi Disemba 2026, ni muhimu kila mmoja wetu kuwa na jukumu la kufuatilia kwa karibu na kuelewa taarifa hizo ili kuanza maandalizi ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na athari za hali ya hewa zinazotarajiwa kujitokeza katika sekta yake, kwa kutambua kuwa upo uwezekano mkubwa kwa El Niño kuendelea kuimarika kuelekea mwishoni mwa mwaka 2026,” alisisitiza Mhe. Jaji Mshibe.


Mhe. Jaji mshibe aliongeza kuwa Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, inaendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayodhihirishwa kupitia ongezeko la joto, ukame, upepo mkali, vimbunga na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko, hivyo amewataka wadau wasiishie katika kupokea taarifa za utabiri wa hali ya hewa, bali wazitumie katika kufanya maamuzi yanayozingatia mazingira ya sekta na maeneo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema TMA imeendelea kuboresha utoaji wa taarifa za hali ya hewa, ikiwemo kuandaa utabiri mahususi kwa maeneo madogo kwa wilaya 86 zilizopo katika mikoa inayopata mvua za Vuli, hatua inayolenga kuhakikisha kila wilaya na sekta husika zinaweza kutumia taarifa za hali ya hewa katika kufanya maamuzi na kupanga shughuli zao.

Comments