TIRDO YAJA NA DAWA ASILI YA MIMEA YA KUCHAKATA NGOZI,HAUTUMII TENA KEMIKALI

 





Na Thadei PrayGod,Dar es salaam 

Shirika la utafiti na maendeleo ya viwanda Tanzania,(TIRDO) limesema limekuja na teknolojia mpya ya kuchakata ngozi bila kutumia kemikali kupitia mimea asili.


Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam kwenye maonesho ya 50 ya kimataifa ya biashara (DITF) yanayofanyika kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu kama sabasaba na mtafiti kutoka Tirdo, Mhandisi Yusufu Sampuli kutoka kitengo cha teknolojia za mvua na ngozi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda la shirika hilo.

Mhandisi Sampuli amesema kuwa ujio wa dawa hiyo ambayo itakuwa mkombozi mkubwa kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na uchakataji wa bidhaa za ngozi za wanyama,ni zao la tafiti zilizofanywa na wataalamu wa shirika. 

"kitu kikubwa ambacho tungependa kuwaambia wananchi ni kwamba,tumeweza kupata dawa ya kuchakata ngozi inayotokana na mimea ambayo mwenyezi Mungu ametubariki kwenye nchi yetu, na hii inatumika kama mbadala wa kemikali za viwandani tunazotumika kuchakata ngozi ili kupata Ile ambayo tunatumia kutengenezea bidhaa mbalimbali ikiwemo mikoba na viatu" amesema mhandisi Sampuli.

Amesema kwa mwaka huu, lengo la shirika kuonyesha teknolojia hiyo, ni ili kuwafahamisha wananchi kuhama kwenye utaratibu wa kutumia kemikali na kuanza kutumia dawa za asili ambazo zinaokoa afya na kulinda mazingira na kuendana na dunia ambayo inapambana kutunza mazingira na afya za watumiaji wa bidhaa mbalimbali.

"soko la bidhaa ambazo zimetengenezwa kwa kutokana na vitu vya asili limeongezeka sana ,sasa hivi hususan mataifa kama ya Ulaya ambayo yanahitaji bidhaa za ngozi iliyochakatwa kwa mimea asili na siyo kemikali kwani bidhaa zitokanazo na kemikali huatarisha usalama wa afya ndo maana unaweza kuvaa viatu ukachubuka ngozi au kupata fangasi" ameongeza.

Aidha ameongeza kuwa,tayari wajasiriamali hasa wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro wameanza kuitumia dawa hiyo kwenye uchakataji wa ngozi, ambapo wamezalisha bidhaa zenye ubora na shirika limeendelea kuwatembelea ili kutambua mafanikio ya dawa hiyo na kama Kuna changamoto,basi itatuliwe.

Hata hivyo mhandisi huyo amewashauri wajasiriamali kufanya vipimo vya kimaabara ili kujua ubora wa bidhaa za ngozi wanazozitengeneza, kwani TIRDO ina maabara ya kisasa ya kupima ubora wa ngozi.


Comments