CHUO CHA DMI CHASISITIZA UWEKEZAJI MKUBWA ELIMU, TEKNOLOJIA:UCHUMI WA BULUU
CHUO CHA DMI CHASISITIZA UWEKEZAJI MKUBWA ELIMU, TEKNOLOJIA,UCHUMI WA BULUU
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Gurumo, amesema Tanzania inahitaji kuongeza uwekezaji katika elimu, teknolojia, rasilimali watu na utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha uchumi wa buluu unakuwa endelevu na unawanufaisha wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla.
Amesema hayo Septemba 9,2026 jijini Dar es salaam wakati akitoa ufafanuzi juu ya baadhi ya mambo yaliyoibuliwa katika Kongamano la Kimataifa la Tano la Uchumi wa Buluu huku akisisitiza kuwa pamoja na kuongeza matumizi ya rasilimali za bahari kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi, ni muhimu pia kuzilinda na kuzitunza ili zisimalizike kutokana na matumizi yasiyo endelevu.
“Tunatambua kwamba tunatazama matumizi bora ya maji tuliyonayo na rasilimali zake kwa faida za kiuchumi, lakini tusije tukajisahau kwamba tusipozitunza rasilimali hizi zinaweza kufikia mwisho na kuisha,” amesema Profesa Gurumo
Aidha amesema kuwa Kongamano hilo limeonyesha kuwa bado kuna fursa nyingi za uwekezaji na ujasiriamali katika uchumi wa buluu zinazohitaji uwezeshaji wa kifedha.
Amesema hali hiyo inazitaka taasisi za fedha kubuni mifumo rafiki itakayowawezesha wajasiriamali kupata mitaji na kukuza shughuli zao katika sekta hiyo.
Aidha,amesema ushirikishwaji wa jamii ni miongoni mwa misingi muhimu ya uchumi wa buluu, hivyo wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka bahari na vyanzo vingine vya maji wanapaswa kupewa elimu kuhusu fursa zilizopo na namna ya kuzitumia kwa njia endelevu.
Profesa Gurumo amesema elimu hiyo inapaswa kuanzia ngazi za jamii, vijiji, mitaa, halmashauri hadi mikoa, huku wataalamu wakishirikiana na Serikali kuwafikia wananchi na kuwaeleza fursa pamoja na wajibu wao katika kulinda rasilimali za bahari.
TEKNOLOJIA
Akizungumzia suala la teknolojia, Profesa Gurumo amesema Tanzania inapaswa kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani, hususan katika taasisi za elimu na mafunzo zinazozalisha wataalamu wa sekta ya bahari.
“Tunahitaji kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili kutoa vijana ambao wanaenda kazini wakielewa wanachokifanya, lakini pia industry iweze kufaidika,” amesema.
Amesema taasisi zinazohusika na elimu na mafunzo ya uchumi wa buluu zinahitaji uwekezaji mkubwa katika mitambo, vifaa na teknolojia za kisasa ili wahitimu waweze kuingia katika soko la ajira wakiwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta ya kimataifa.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo unapaswa pia kuwahusisha wakufunzi na wataalamu, ikiwa ni pamoja na kuwezesha ushirikiano na taasisi za elimu kutoka nchi ambazo zimepiga hatua katika sekta ya bahari.
SHERIA, MIKATABA
Kwa upande wa sheria na sera, Profesa Gurumo amesema kongamano hilo limebaini umuhimu wa kuhakikisha mikataba na sheria za kimataifa zinazohusu bahari zinaridhiwa na kutekelezwa kikamilifu.
Amesema sambamba na hilo, Tanzania inahitaji kuwa na sheria na miongozo ya ndani inayowezesha nchi kunufaika na rasilimali za bahari, huku ikihakikisha zinatumika kwa uendelevu.
Ameutaja Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria za Bahari (UNCLOS) kuwa miongoni mwa misingi muhimu inayotoa mwongozo kuhusu maeneo ya bahari, ikiwemo Territorial Sea na Exclusive Economic Zone (EEZ), pamoja na matumizi na uhifadhi wa rasilimali za bahari.
Aidha, amesema Agenda ya Afrika ya Maendeleo 2063 imeweka msisitizo katika matumizi ya rasilimali za bahari na uchumi wa buluu, hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuongeza kasi ya kuridhia na kutekeleza mikataba na mipango inayolenga kukuza sekta hiyo.
Profesa Gurumo amesema maazimio ya kongamano hilo yameweka msisitizo mkubwa katika elimu kwa jamii na ujenzi wa rasilimali watu, akibainisha kuwa bado wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu uchumi wa buluu na fursa zake.
Amesema elimu na uelewa huo ni muhimu ili wananchi wawe sehemu ya juhudi za kutumia rasilimali za bahari kwa manufaa ya kiuchumi bila kuziharibu kwa matumizi yasiyo endelevu.



Comments