JUMUIYA YA WAISLAM WAAHMADIYYA TANZANIA KUFANYA MKUTANO MKUU WA 55,KITONGA DAR,YAWAITA WATANZANIA
DAR ES SALAAM:
Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa mwaka (Jalsa Salana)wa 55 kuanzia Septemba 25 hadi 27, 2026, katika eneo la Kitonga, Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam,huku zaidi ya washiriki 5,500 wakitarajiwa kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam,Amiri na mbashiri mkuu wa Jumuiya hiyo,Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad amesema mkutano huo wa kila mwaka unalenga kuwaimarisha waumini katika masuala ya kiroho, ikiwemo kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu mioyoni mwao, kupata Taqwa (uchamungu), kumjali Mwenyezi Mungu, kujiepusha na mambo mabaya, kuwa na moyo wa huruma na kuongeza upendo baina yao.
Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu “TAQWA (UCHAMUNGU) NDIO MSINGI WA KILA WEMA”, ikiwa na lengo la kuwakumbusha waumini umuhimu wa kuishi kwa maadili ya dini na kufanya mema.
Sheikh Khawaja ameongeza kuwa, katika mkutano huo kutajadiliwa pia changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia, ikiwemo migogoro na vita katika maeneo mbalimbali, huku ikieleza kuwa Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zinazohifadhi wakimbizi kutokana na migogoro hiyo.
"waumini watapata fursa ya kushiriki katika ibada mbalimbali, ikiwemo Sala ya pamoja ya usiku (Tahajjud), ambayo inatajwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya mkutano huo. Pia kutakuwa na mihadhara na mafundisho yanayolenga kuongeza imani na uelewa wa dini" amesema.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya ni jumuiya ya kimataifa inayodai kuwa na uwepo katika nchi 212 duniani, chini ya uongozi wa Khalifa wa Jumuiya hiyo, Hadhrat Mirza Masroor Ahmad.
Aidha, viongozi wa Jumuiya hiyo wamewahimiza waumini kushiriki katika shughuli za kusaidia jamii, ikiwemo kuwafikia watu wenye mahitaji na kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Mkutano huo pia utatumika kuhimiza waumini kuendelea kushikamana, kudumisha amani na kuishi kwa kufuata misingi ya dini, huku wakizingatia kauli mbiu ya mkutano ya “Taqwa (Uchamungu) ndio msingi wa kila wema.”



Comments