Skip to main content

ZAIDI YA WATU ELFU 48 WAPIGA KURA TUZO ZA TMA, KIPENGELE CHA MWANAMUZIKI BORA CHIPUKIZI CHAONGOZA

 

ZAIDI YA WATU ELFU 48 WAPIGA KURA TUZO ZA TMA, KIPENGELE CHA MWANAMUZIKI BORA CHIPUKIZI CHAONGOZA



Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU. 

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema mwamko wa upigaji kura wa Tuzo za Muzika Tanzania (TMA) ni mkubwa kwamba hadi sasa zaidi ya watu elfu 48 wameshapiga kura.

Hayo yamebainiahwa leo Aprili 14, 2023 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa BASATA Dkt. Kedmon Mapana akizungumza na waandishi wa habari kueleza mwenendo wa upigaji kura wa tuzo hizo uliofunguliwa Aprili 8 mwaka huu.

“Watanzania mpaka sasa wana mwamko mkubwa wa kupiga kura, hadi dirisha la upigaji kura mwaka jana linafungwa watu waliokuwa wamepiga kura ni elfu 84, lakini kwa mwaka huu ndani ya siku sita leo zaidi ya watu elfu 48 wameshapiga kura,” amesema Dkt. Mapana na kuongeza,

“Huu ni mwamko mzuri naamini hadi tarehe 28 mwaka huu tutakuwa na wapiga kura wengi, hivyo tunajivunia kwa jambo hili,”.

Ametaja vipengele vinavyoongoza kupigiwa kura ni kipengele cha mwamuziki bora chipukizi ambacho kina ziadi ya kura 2000 na mwimbaji bora wa kiume kura zaidi ya 1900.

Vipengele vingine ni mwimbaji bora wa kiume wa Bongo Fleva kura zaidi ya 1900 na mwimbaji bora wa kike wa Bongo Fleva kura zaidi ya 1500.

Hivyo Dkt. Mapana ameeleza kwamba kupigiwa kura kwa wingi kipengele cha manamuziki bora chipukizi ni ishara nzuri katika uandaaji wa wasanii wakubwa wajao.

Dkt. Mapana ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kupiga kura kwani dirisha la upigaji kura litafungwa Aprili 28, mwaka huu na Tuzo zenyewe zitafanyika Aprili 29 mwaka huu.

Comments