HESLB NA TRA KUSHIRIKIANA KUWABAINI WANUFAIKA WA MIKOPO WALIO SEKTA ISIYO RASMI AMBAO HAWAJAIREJESHA

 HESLB NA TRA KUSHIRIKIANA KUWABAINI WANUFAIKA WA MIKOPO WALIO SEKTA ISIYO RASMI AMBAO HAWAJAIREJESHA.



NA MWANDISHI WETU

Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini,HESLB Leo imebadilishana hati za ushirikiano baina yake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),ikiwa ni muendelezo wa kuboresha huduma zake  kuwafikia wanufaika wa mikopo hiyo.


Akizungumza katika hafla fupi ya kubadilishana hati za ushirikiano Kati ya bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na wadau wa kimkakati iliyofanyika Leo Septemba 13,2024 Jijini Dar Es Salaam,Mkurugenzi mtendaji wa HESLB Dkt Bill Kiwia amesema lengo la kukabidhiana hati hizo ni ili kuwafikia wanufaika wa mikopo walio katika sekta isiyo rasmi ambao wana kipato na hawajarejesha mikopo yao.


Amesema kupitia ushirikiano huo Sasa bodi ya mikopo itaboresha huduma zake kwa urahisi na kuwafikia wanufaika wa mikopo kupitia kanzidata za TRA ambao watatoa taarifa za wanufaika wa mikopo ambao hawajairejesha ili wanufaika wengine walio vyuoni nao wapate.


"Jambo hili tunalolifanya hapa Leo pia litachangia sisi HESLB na TRA kubadilishana uzoefu baina yetu na kuwafanya wale wasiorejesha mikopo yao ambao hawapo kwenye ajira rasmi lakini wana kipato kupitia sekta isiyo rasmi,kurejesha Mikopo"amesema Dkt Kiwia


Aidha amewasisitiza wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao bado hawajaanza kurejesha Mikopo yao,kurejesha tena kwa wakati ili kufanya bodi kuwa na uwezo mkubwa wa kuwapa wengine.


Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Yusuph Mwenda ameipongeza bodi hiyo kwa kazi kubwa ya utoaji mikopo kwa wanafunzi wa kitanzania ambayo imechangia pakubwa katika kukua kwa sekta ya elimu nchini.


"Kile wanachofanya bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ni matokeo ya watanzania kulipa Kodi na hatimaye Kodi hizo pia kutumika kugharamia bodi katika utoaji mikopo kwa watoto wetu wa kitanzania" amesema Mwenda


Hata hivyo Kamishna huyo amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), itakuwa mstari wa mbele kubadilishana taarifa na bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu(HESLB) ili kuhakikisha wanufaika wa mikopo ambao wako sekta isiyo rasmi wanarejesha mikopo hiyo.

Comments