SERIKALI KUVUTIA WAWEKEZAJI UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI- DKT. BITEKO

 SERIKALI KUVUTIA WAWEKEZAJI UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI- DKT. BITEKO






📌 *Ashuhudia makabidhiano leseni  ya uendelezaji Gesi Asilia Kisima cha Ruvuma*


📌 *Azitaka TPDC na ARA Petroleum kutoa kipaumbele kwa wazawa katika ajira*


📌 *Kitalu cha Ruvuma kuzalisha Gesi futi ujazo trilioni 1.6*




 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji katika tafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini ili watanzania wanufaike na rasilimali zilizopo.


Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 10, 2024 wakati wa Hafla ya makabidhiano ya leseni ya uendelezaji eneo la uzinduzi wa Gesi kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na ARA Petroleum katika kisima cha Ruvuma Ntorya mkoani Mtwara. 


"Yote haya mnayoyaona ni matunda ya kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan." Amesema Dkt.Biteko


Ameongeza kuwa, jitihada za Serikali zinaenda sambamba na kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili liweze kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa thamani wa Mafuta na Gesi.


Aidha, ametoa wito kwa TPDC na kampuni ya ARA Petroleum kutoa kipaumbele kwa 

wazawa  katika utoaji wa ajira ili kuwe na muunganiko kati ya wananchi na ukuaji wa uchumi katika  maeneo hayo.


Kuhusu maeneo yenye miradi ya Gesi kama Madimba, Msimbati na Songosongo  amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha upelekaji wa umeme kwenye maeneo hayo kufikia mwezi Desemba mwaka huu.


Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,  Mhe. Kirumbe Ng'enda amesema utoaji wa leseni ya uendelezaji kitalu cha gesi cha Ruvuma ni hatua kubwa  maendeleo nchini. 


"Kitalu hiki kitazalisha futi za ujazo trilioni 1.6, hili ni jambo kubwa sana na la kuipongeza Serikali, tunampongeza Rais Samia ambaye yeye ndie jemedari wa mapambano ya kuleta maendeleo nchini.' Amesema  Mhe Ng'enda


Aidha kutokana na uwepo wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere ambao hivi sasa unachangia takribani megawati  705 kwenye gridi ya Taifa, Ng'enda ameiasa Serikali kuwa  gesi hiyo  sasa itoe mchango mkubwa katika nishati safi ya kupikia na katika uendeshaji wa mitambo na kwenye magari.


Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,  Mha. Felchesmi Mramba alisema kuwa Tanzania ina historia ndefu katika matumizi ya Gesi Asilia kuanzia miaka ya sabini baada ya ugunduzi katika visiwa vya Songosongo. 


Ameongeza kuwa,  ugunduzi wa Gesi Asilia umefungua mlango endelevu wa uhifadhi wa mazingira na kuimarika kwa usalama wa nishati.

Comments