Skip to main content

WMA YAHIMIZA USHIRIKIANO KUTOKA SEKTA BINAFSI

 

WMA YAHIMIZA USHIRIKIANO KUTOKA SEKTA BINAFSI

 










 *Mahamudu Jamal na Pendo Magambo, WMA*


Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla ametoa wito kwa taasisi, asasi na mashirika binafsi kuimarisha ushirikiano na Wakala hiyo katika masuala yanayohusu vipimo kwa nyanja za biashara, afya, usalama na mazingira.


Kihulla ametoa wito huo leo Septemba 11, 2024 alipokuwa akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, na kufanyika jijini Dar es Salaam.


Akitoa taarifa ya utendaji kazi, majukumu pamoja na mafanikio ya WMA, amesema kuwa kuna maeneo zaidi ya 17 ambayo sekta binafsi inaweza kushirikiana na WMA ili kuongeza tija katika sekta ya vipimo nchini.


Ametaja baadhi ya maeneo hayo ya kivipimo kuwa ni pamoja na ukaguzi na uhakiki wa mizani, uhakiki wa mitambo ya gesi, dira za maji zilizopo kwenye matumizi, mashine za michezo ya kubahatisha, lifti za majengo na maeneo mengine.


Akizungumzia Sheria inayoipa Mamlaka WMA kutekeleza majukumu yake, Mtendaji Mkuu amesema sheria hiyo ambayo msingi wake hasa ni vitabu vitakatifu vya dini Quran na Biblia, ni ya Usimamizi wa Vipimo Sura Namba 245 na 340 ya Mwaka 2002 ambayo inawatambua Maafisa Vipimo kama mainspekta wakati wanapotekeleza majukumu ya ukaguzi na uhakiki wa vipimo.


Amebainisha kuwa, jukumu kubwa la WMA ni kuilinda jamii ili kuepukana na madhara yatokanayo na matokeo ya upimaji usio sahihi katika biashara ambapo WMA inawajibika kukagua sehemu za biashara kama vile maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali, viwanda, maduka ya vifaa vya ujenzi, vituo vya kujazia mafuta na sehemu nyinginezo.


“Tunasisitiza kila mara kwa wananchi kuwa ukihisi kwamba umepimiwa visivyo sahihi katika sehemu uliyoenda kupata huduma, ni jukumu lako kutoa taarifa ili wataalamu wetu wakafanye uchunguzi eneo hilo.”


Aidha, ameongeza kuwa WMA inawajibika kuhakiki mzunguko mzima wa mafuta kuanzia yanapoingia nchini kupitia bandari, uhakiki wa matanki na maghala ya kuhifadhia mafuta ambapo Wakala hufanya shughuli hizo kupitia kitengo maalum cha Bandari “Port Unit”.


Sanjari na hayo, Kihulla ameweka wazi kuwa WMA ina mpango wa kuingia kwenye maeneo mapya ya uhakiki wa vipimo kama vile uhakiki wa gharama za vifurushi vya muda wa maongezi na mashine za michezo ya kubashiri (gaming).


Pia, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa vipimo kuhusiana na matakwa ya sheria ya vipimo, kuendelea kuboresha mifumo ya utendaji kazi pamoja na kuwajengea uwezo zaidi wataalamu wake ikiwa ni kuwapa mafunzo zaidi na ununuzi wa vifaa vya kisasa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameipongeza WMA kutokana na utendaji kazi wake na ameahidi ushirikiano wa vyombo vya habari na Wakala hiyo ili kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi ya vipimo inawafikia wananchi kwa ukubwa wake.


“WMA mna nafasi ya kuufikia umma wa watanzania kwa kutumia vyombo vya habari kwenye kampeni hizi za kivipimo, elimu inahitajika sana, wananchi wanatakiwa kufahamu kwamba wanapaswa kuwa makini wanapokwenda kupata huduma mbalimbali, hii itachagiza maendeleo katika taifa letu” amesisitiza Balile.


WMA imeendelea kutoa elimu ya vipimo kwa wadau wake mbalimbali ambao ni pamoja na taasisi za umma na binafsi na pia kuwa mstari wa mbele katika kuchangia katika Pato la Taifa kupitia uwasilishaji wa gawio la Serikali kwa Msajili wa Hazina ambapo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, ilitunukiwa Tuzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Comments