MAADHIMISHO ya Siku ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa mwaka huu, yatafanyika kesho Oktoba 24, 2024 katika Viwanja vya Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Dar es salaam

 MAADHIMISHO ya Siku ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa mwaka huu, yatafanyika kesho Oktoba 24, 2024 katika Viwanja vya Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Dar es salaam 




Dar es salaam

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 23, 2024 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Cosato Chumi akizungumza na waandishi wa habari


Chumi amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni, "Ustawi wa Vizazi Vijavyo, Kuchochea Ukuaji wa Uchumi Endelevu Tanzania". 


"Kaulimbiu hii ni kielelezo cha ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa, unaozingatia maendeleo endelevu ambayo yananufaisha sio tu kizazi kilichopo bali pia vizazi vijavyo," amesema Chumi na kuongeza,

 


"Kama ilivyo ada, maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa hufanyika tarehe 24 Oktoba kila mwaka, ikiwa ni kumbukumbu ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa (entry into force of the UN Charter) na kuanza kazi rasmi kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945," 


Hivyo amebainisha kuwa, haya ni maadhimisho ya 79 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mfumo wa Umoja wa Mataifa nchini ya kuadhimisha siku hii adhimu. 


Kwamba hafla hiyo itahusisha kupandishwa kwa Bendera ya Umoja wa Mataifa katika viwanja vilivyopo Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Jengo la PSSSF, Barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam. 


Amesema kupandishwa kwa Bendera ya Umoja wa Mataifa ni ishara na kielelezo kwamba Tanzania imedhamiria kwa dhati, kuendelea kuheshimu na kudumisha misingi, malengo na tunu za Umoja wa Mataifa, ikiwemo amani, umoja, haki, usawa, utu, maendeleo na ustawi kwa watu wote.   


Naibu Waziri Chumi ameeleza kuwa

Tanzania imekuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya miaka 60 na kwamba katika kipindi chote hiki, imeendelea kuheshimu misingi, malengo na tunu za Umoja wa Mataifa.


Amesema zaidi ya kuziheshimu, pia imezitetea kwa kushiriki ipasavyo katika jitihada za ulinzi wa amani, sehemu mbalimbali duniani; kuimarisha ushirikiano katika kuwatafutia watu wetu maendeleo endelevu na kulinda haki za binadamu. 


"Tumetekeleza wajibu huu, katika vipindi mbalimbali, ikiwemo wakati wa Vita Baridi, vilivyochagizwa na uhasama baina ya nchi za magharibi na mashariki. Tumetekeleza wajibu huu kwa gharama kubwa, ikiwemo kupoteza mashujaa wetu kwenye operesheni za ulinzi wa amani na usalama katika nchi mbalimbali," ameongeza Chumi.


Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono dhamira njema ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa na itaendelea kujitoa zaidi kutetea Umoja huu, misingi, malengo na tunu zake kwa ustawi wa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo. 


Kwa upande wake, Kaimu Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Mark Bryan Schreiner amesema zaidi ya hayo, maadhimisho haya yanarandana na makubaliano ya Mkutano wa Baadae, ambayo yanasisitiza juu ya ushirikiano wa kimataifa katika kushughulikia changamoto mbalimbali za kidunia, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, matumizi hasi ya teknolojia na akili mnemba, na umaskini, migogoro na magonjwa ya mlipuko.


"Umoja wa Mataifa unasimamia amani, haki na kubeba matumaini ya binadamu wote. Tunaadhimisha miaka 79 ya Umoja wa Mataifa, tukitambua kuwa shirika hili liko kwenye shinikizo kubwa, na linakabiliana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake, hasa yanayohusiana na kudumisha amani na usalama wa kimataifa, na ukiukwaji wa haki dhidi ya wafanyakazi wake, hasa wale wanaohudumu katika operesheni za kulinda amani. Licha ya changamoto zake nyingi, ukweli wa msingi unabaki kwamba shirika hili la kimataifa lina kusudi muhimu na nafasi adhimu ya kufanya mambo makubwa zaidi kwa ustawi wa nchi zote wanachama. Hivyo, Tanzania itaendelea kuwa mwanachama hai na mwadilifu wa Umoja wa Mataifa katika jitihada zake za kujenga dunia yenye amani, haki, mafanikio na salama kwa watu wote.”


"Tunapoadhimisha miaka 79 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, tunasherehekea ushirikiano wa kudumu kati ya Serikali na watu wa Tanzania na Umoja wa Mataifa," alisisitiza kaimu Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bw. Mark Bryan Schreiner. "Kauli mbiu ya mwaka huu, Ustawi wa Vizazi Vijavyo: Kuchochea Ukuaji wa Uchumi Endelevu Tanzania, inaonyesha dhamira ya pamoja ya kufikia maendeleo endelevu na kuhakikisha mustakabali mzuri kwa wote."

Comments