Dkt Mpango Akaribisha Wawekezaji Kuwekeza katika Nishati ya Jotoardhi Tanzania

 Makamu wa Rais Akaribisha Wawekezaji Kuwekeza katika Nishati ya Jotoardhi Tanzania









DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ametoa mwaliko kwa wawekezaji kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza miradi ya nishati ya jotoardhi inayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Dkt. Mpango alibainisha maeneo muhimu yenye uwezo wa kuzalisha nishati ya jotoardhi. Miongoni mwa maeneo hayo ni Ngozi (MW 60), Kyejo – Mbaka (MW 60), Songwe (MW 5-35), Natron (MW 60), na Luhoi (MW 5).


Dkt. Mpango alieleza kuwa Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji katika sekta hii kutokana na mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji, utulivu wa kisiasa, na sera imara. Alisisitiza kuwa uboreshaji wa sekta mbalimbali unafanywa chini ya falsafa ya "R Nne" ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inalenga mageuzi, kujenga upya, maridhiano, na ustahimilivu.


Aidha, Makamu wa Rais aliwataka wanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopitiwa na Bonde la Ufa (ARGeo) kushirikiana katika juhudi za kuchunguza rasilimali za jotoardhi na kuvutia uwekezaji. Alisisitiza umuhimu wa kubadilishana maarifa, teknolojia, na mbinu bora, pamoja na kuunda na kutekeleza programu za kikanda za utafiti wa jotoardhi.


Pia, alitoa wito kwa nchi wanachama kuwa na taasisi maalum zinazoratibu maendeleo ya jotoardhi na kuhakikisha uwepo wa mifumo madhubuti ya kisheria na udhibiti, ambayo itatoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa jotoardhi.


Makamu wa Rais aliongeza kuwa kutokana na changamoto za kifedha, bajeti za serikali pekee haziwezi kugharamia miradi mikubwa ya jotoardhi. Hivyo, alizihimiza nchi wanachama wa ARGeo kuwa na mazungumzo na mashirika ya fedha ya kimataifa, kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia, ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi.


Kwa sasa, Tanzania imekamilisha hatua za awali za utafiti wa rasilimali za jotoardhi katika maeneo matano kando ya bonde la ufa, na utafiti wa kina umeanza katika Ziwa Ngozi, Magharibi mwa Tanzania. Miradi mingine inayofanyiwa uchunguzi ni Kyejo-Mbaka, Luhoi, na Natron. Mafanikio mengine yaliyoelezwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wataalam wa jotoardhi nchini na ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima.


Kongamano hilo la siku saba lina kaulimbiu "Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi Afrika," na linahusisha washiriki 800 kutoka mataifa 21 duniani.

Comments