NI SAMIA KALAMU AWARDS 2024,MUDA WA KUWASILISHA KAZI KUSHIRIKI TUZO ZA HABARI ZA MAENDELEO WASOGEZWA MBELE

 NI SAMIA KALAMU AWARDS 2024,MUDA WA KUWASILISHA KAZI KUSHIRIKI TUZO ZA HABARI ZA MAENDELEO WASOGEZWA MBELE


Na Mwandishi wetu ,Dar es Salaam 

CHAMA cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameongeza muda wa maombi ya ushiriki katika Tuzo za Samia Kalamu Awards hadi Oktoba 30, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa Dkt. Rose Reuben amesema awali tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ilikuwa Oktoba 26, mwaka huu.

Amesema uamuzi wa kuongeza muda umechukuliwa ili kutoa nafasi kwa wale waliokutana na chagamoto za kiufundi, ikiwemo kushindwa kuipandisha kazi mtandaoni kutokana na matatizo ya mtandao na chagamoto nyingine.

"Tunapenda kuwataarifu waandishi wa habari, vyombo vya habari, maafisa habari na wadau wa habari kuwa muda wa kuomba kushiriki katika tuzo umesogezwa mbele hadi Octoba 30,2024 "amesema 

Dkt Rose amesema  Tuzo hizo zitatolewa kwa wanahabari wa kitanzania zikiwa na lengo la kuhamasisha, kukuza na kupanua wigo wa uandishi, utangazaji na uchapishaji wa maudhui ya ndani, kupitia vyombo vya habari vya asili na mitandaoni, ili kuchochea uandishi wa makala za kina zinazozingatia maendeleo.


Aidha amewaomba wale wote ambao awajawasilisha kazi zak kuchukua hatua za haraka na kufanya hivyo kabla kufikia Octoba 30, 2024 .

"Hii ni fursa adhimu kwa vyombo vya habari, waandishi wa habari, maafisa habari kuonesha umahiri wao wa kuchakata habari na kuthaminiwa Kwa michango yao katika taaluma ya uandishi"amesema Dkt Rose 

Dkt Rose alisisitiza kuwa  kazi zinazowasilishwa zinatakiwa kuwa za kipekee na ambazo hazijawahi kuwasilishwa kuwania tuzo nyingine, na zinazofuata taratibu za haki miliki. Waandishi wanatakiwa kuwasilisha kazi zao kupitia tovuti rasmi ya www.samiaawards.tz

Kwa upande wa takwimu za maombi ya tuzo Dkt Rose amesema hadi Oktoba 23, mwaka huu wamepokea maombi kutoka mikoa 23 ya Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Mwanza, Mtwara, Simiyu, Geita, Njombe, Mbeya, Songwe,Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora, Kagera, Mjini Magharibi, Ruvuma, Lindi, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro na Pwani.

Vilevile amesema mchakato wa upigaji kura Kwa wananchi inatarajia kuanza rasmi Novemba 8 mwaka huu hivyo aliwahimiza  wanahabari kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhim wa kushiriki katika upigaji kura kwa wingi, kwani kura za wananchi zinachangia asilimia 60 ya alama za mshindi, huku asilimia 40 zikiamuliwa na jopo la majaji. 

Dkt Rose amesema Wananchi wataweza kupiga kura kupitia namba maalumu ya SMS SHORT CODE 15200 au kwa kutumia tovuti rasmi,”amesema Dk.Rose.

Kwa  upande wake Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA,Mhandisi Andrew Kisaka amesema tuzo hizo ni muhimu kwa ajili ya kukuza na kutambua mchango wa waandishi wa habari katika masuala mbalimbali yakiwemo ya maendeleo.

"Nawahimiza  wanahabari kutoka redioni, televisheni na mitandao ya kijamii kuziwasilisha kwa haraka katika kipindi hiki kilichobaki kwani tunaamini zimeleta mabadiliko chanya kwenye jamii,”amesema Mhandisi Kisaka.

Comments