WATUMISHI HOUSING YATWAA TUZO YA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU AFRIKA

 WATUMISHI HOUSING YATWAA TUZO YA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU AFRIKA


NA PRAYGOD THADEI

Kufuatia kuwa na utoaji wa huduma za nyumba za gharama nafuu na zinazokidhi viwango,Watumishi Housing Investment (WHI) imeshinda tuzo ya Nyumba za Gharama Nafuu Bora Afrika, iliyoandaliwa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika (Africa Union for Housing Finance – AUHF), taasisi inayotambuliwa na Umoja wa Afrika.



Akitangaza ushindi huo jijini Dar es Salaam tarehe 23 Oktoba 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Dkt. Fred Msemwa, alisema tuzo hiyo ilitolewa kwenye mkutano mkuu wa AUHF uliofanyika Zanzibar hivi karibuni.


Dkt. Msemwa alisema kuwa tuzo hiyo ni ishara ya kutambua juhudi za WHI katika kusaidia wananchi wa kipato cha chini na kati kumiliki nyumba nchini Tanzania.


"Juhudi zetu za kuleta mifumo ya malipo nafuu, kama malipo endelevu bila riba yanayofanywa wakati wa ujenzi, pamoja na mpango wa mpangaji mnunuzi, zilitajwa kama sababu kuu za ushindi wetu," alisema Dkt. Msemwa.


Aliongeza kuwa mipango hiyo imewezesha watu wengi kumiliki nyumba kwa gharama ya chini zaidi, ikiwa ni punguzo la asilimia 10 hadi 30 ya bei ya soko, ambapo nyumba zinauzwa kuanzia shilingi milioni 38.


"Tuzo hii imekuja wakati muafaka, tukiadhimisha miaka 10 ya ubunifu na uongozi katika sekta ya makazi," alisema Dkt. Msemwa.




WHI, taasisi ya umma chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, imekuwa ya kwanza katika Afrika Mashariki kushinda tuzo hii ya heshima, ikipongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza sekta ya makazi barani Afrika.


Tuzo za AUHF zinatambua juhudi kubwa katika kuimarisha sekta ya makazi Afrika, na ushindi wa WHI unatokana na ubunifu wao wa miradi ya nyumba za gharama nafuu, hatua ambayo imewasaidia watanzania wengi, hususan watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, kumiliki nyumba.


AUHF ni taasisi ya kimataifa iliyodumu kwa zaidi ya miaka 40, ikiwaleta pamoja wadau wa sekta ya makazi barani Afrika, huku ikiwezesha maendeleo ya ufumbuzi wa makazi kwa bei nafuu.




Comments